Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam Muliro Muliro
……………………………
NA MUSSA KHALID
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam limekanusha ujumbe na video ambayo imekuwa ikisambazwa katika baadhi ya Vyombo vya Habari ikiwemo mitandao ya kijamii ikionesha kikundi cha wahalifu wakivamia magari yaliyokuwa kwenye foleni juu ya Daraja na kufanya vitendo vya kihalifu kama unyang`anyi.
Kwa Mujibu wa taarifa ambayo imetolewa leo na Kamanda wa Jeshi hilo ACP Muliro Muliro amesema wasambazaji wa taarifa hizo wamedai kuwa eneo hilo ni Daraja la Selander ambalo lipo mpakani mwa Ilala na Kinondoni jijini Dar es Salaam jambo ambalo taarifa hizo si sahihi,na sio za kweli ila zina lengo la kujenga hofu na taharuki kwa wananchi .
Kamanda Muliro amesema eneo la Selander usalama wake umeimarishwa kwa kiwango cha juu na maeneo mengine na kueleza kuwa,tukio hilo linalosambazwa lilitokea jijini Gaborone nchini Botswana tarehe 11.2.2022 na Jeshi la Polisi la nchi hiyo kupitia CCTV CAMERA zilizoko barabarani zilinasa picha hizo na zikarushwa kupitia ukurasa wa face book wa Jeshi hilo kuomba wananchi wa maeneo yale kusaidia kwatambua wahalifu wale ili wakamatwe.
Aidha Kamnda Muliro amesema kitendo cha mtu/watu kuchukua taarifa hiyo, kuigeuza na kuanza kuisambaza ni kosa na kinyume na Kifungu namba 16 cha Sheria ya Mtandao ya mwaka 2015 (Section 16 of The Cyber Crime Act,
2015). ambapo kimeeleza kuwa ni kosa la jinai kwa mtu yeyote kusambaza ujumbe wa maandishi wa uongo, Picha, alama au kwa njia ya mfumo wowote katika mtandao
‘Kifungu hicho pamoja na mambo mengine kimeeleza kuwa ni kosa la jinai kwa mtu yeyote kusambaza ujumbe wa maandishi wa uongo, Picha, alama au kwa njia ya mfumo wowote katika mtandao huku akijua ujumbe au picha hiyo inapotosha kwa lengo la kujenga hofu katika jamii. Na endapo atapatikana na hatia Mahakamani atatakiwa kulipa faini ya Tshs milioni tano au kwenda jela miaka isiyopungua mitatu au vyote kwa pamoja’.
Hata hivyo Jeshi hilo limewatahadharisha wanaofanya vitendo hivyo na kuwa litafuata mifumo ya kisheria ili kushughulika na mambo kama hayo kwa watu watakaobainika kusambaza video hizo