Binti Rose Deogratius mwenye umri wa miaka 12 ambaye ni mwanafunzi wa darasa la Saba katika shule ya msingi ya Kimara Baruti anapambana kuyapigania maisha yake akiwa kitandani katika hospitali ya Taifa Muhimbili.
Rose ansumbuliwa na tatizo la kushambuliwa vibaya kwa mishipa yake ya moyo iliyopelekea kushindwa kutembea na hivyo kushindwa kabisa kuendelea na masomo yake lakini kwa ukuu wa Mungu aliweza kufanya mtihani wake wa darasa la sita akiwa kitandani na kufaulu.
Hali ya Rose imezidi kuwa mbaya, tangu shule zifunguliwe hajaweza kuudhuria masomo yake akiwa darasani kutokana na mwili wake kudhoofu na sura yake kuvimba huku akibebwa muda wote kutokana na mwili wake kukosa nguvu ya kuweza kufanya chochote.
Rose anahitaji kufanyiwa upasuaji utakaoweza kumaliza tatizo lake lakini gharama za matibabu yake ili kufanyiwa upasuaji huo zimekuwa kubwa kwake na hivyo kuzidi kutishia uhai wake anaoupigania akiwa kwenye kitanda cha wodi ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete jijini Dar.
Gharama za kumtibu mtoto Rose zinazohitajika hospitalini ni shilingi Milioni Kumi na Mbili na Laki Nane (12,800,000) huku wazazi wake wakiwa na kiasi cha shilingi Milioni Mbili (2,000,000) tu na hivyo kuomba msaada kwa wasamaria wema kuweza kuwasaidia kufikia lengo hilo na hivyo kuunusuru uhai wa binti yao.
Tafadhali tunaombwa kuchangia gharama za matibabu ya mtoto Rose kwa kutuma chochote tutakachojaaliwa kupitia namba ya simu ya Mama yake mzazi 0653 302 811 (Monika Kobe) ili mtoto Rose aweze kufanyiwa upasuaji utakaomaliza tatizo lake na hivyo kuendelea na masomo pamoja na kuweza kuunusuru uhai wake.
Mungu akubariki sana.