Kwa mara nyingine tena, Benki ya NMB imeonyesha ni benki inayojali watu wa hali zote kiuchumi na kijamii, na leo imeungana na Shirikisho la Umoja wa Machinga Tanzania (SHIUMA) katika kuhakikisha wafanyabiashara wenye mitaji midogo wanakua kibiashara.
Akizungumza na waandishi wa habari katika hafla ya kutiliana saini makubaliano hayo jijini Dar es Salaam, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara NMB, Filbert Mponzi alisema benki hiyo ni kinara wa kushirikiana na wajasiriamali wa viwango vyote nchini.
Alibainisha kuwa mbali ya kutoa mikopo na mafunzo ya biashara, NMB kwa kushirikiana na kampuni ya bima ya Reliance watatoa huduma ya bima itakayolinda biashara za wamachinga dhidi ya majanga kama moto, ajali na mafuriko.
Bima hiyo itaanzia Shilingi 10,000 kwa mwaka ambapo mnufaika atapata hadi Sh 500,000. Lakini pia kuna bima ya Sh 60,000 kwa mwaka ambapo mnufaika atapata hadi Shilingi Milioni 10 pale atakapopatwa na majanga yaliyoainishwa.
Pia, Mponzi alisisitiza kuwa NMB inathamini juhudi za Wajasiriamali Wadogo Wadogo (SME’s) na kwa kuonyesha hilo imejikita zaidi katka kuhakikisha shughuli zao zinakua nchini na ndio maana imekuwa ikitoa mchango mkubwa kuwezesha sekta hiyo muhimu kibiashara nchini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shirikisho la Umoja wa Machinga Tanzania (SHIUMA), Ernest Masanja alisema benki ya NMB imewasaidia kwa kiasi kikubwa katika masuala mbalimbali ikiwemo mitaji na fursa za kukua kibiashara kwa miaka mingi.
Mkurugenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maluum, Juma Samwel alisema anaishukuru benki ya NMB na SHIUMA kwa makubaliano hayo ya kihistoria ya miaka mitano kwa kuwa wizara inatambua kupitia makubaliano hayo wmachinga wataendelezwa kiuchumi na kuongeza fursa za kibiashara. Lakini pia alibainisha kuwa wamachinga wote nchini watakuwa na ujuzi sawa kupitia mafunzo watakayopewa.
Itakumbukwa tangu mwaka 2000 benki ya NMB imekuwa ikitoa mikopo midogo kuanzia Sh 50,000 hadi Sh Mil 50.