Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani Nchini (FCC), William Erio akizungumza wakati alipokuwa akifungua semina ya Jumuiya ya wafanyabiashara wa Kariakoo iliyofanyika leo kwenye ofisi za FCC Posta jijini Dar es Salaam.
Picha mbalimbali zikionesha wafanyabiashara wakiwa katika semina hiyo iliyofanyika leo kwenye ofisi za FCC Posta jijini Dar es Salaam.
…………………………………………
NA JOHN BUKUKU DAR ES SALAAM
Lengo kubwa la Tume ya Ushindani wa Kibiashara (FCC) ni kuimarisha biashara kwa kutoa elimu na kushirikiana vyema na wadau zikikiwemo taasisi kama TBS, BRELA, TRA na wadau wengine pamoja na Wafanyabiashara nchini kote na sio kuwakwamisha wafanyabiashara hao wasiendelee katika kufanya biashara zao.
Wafanyabishara nchini ni muhimu wakatumia vyema elimu waliyoipata kutoka FCC na kueleza wazi athari za bidhaa bandia ambazo ni hatari sana zinapoingia katika soko na kukwamisha ukuaji wa uchumi wa taifa.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani Nchini (FCC), William Erio alipowakaribisha wafanyabiashara wakati akifungua semina ya iliyofanyika kwenye ofisi za FCC zilizopo mtaa wa Sokoine jijini Dar es Salaam.
Bw. William Erio aliwataka wafanyabiashara nchini kuwafichua wale wanaojihusisha na uzalishaji na usambazaji wa bidhaa bandia, ili wachukuliwe hatua za kisheria kwa sababu matendo wanayoyafanya yanadidimiza uchumi wa taifa na kuwakwamisha wafanyabiashara nchini.
Ameongeza kuwa FCC itaendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara wote nchini, ili wajue athari za bidhaa bandia katika ukuaji wa uchumi nchini.
“Naipongeza jumuiya hiyo ya Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo (JWK) kwa kuhudhuria kwa wingi katika semina hii kwa sababu watapata elimu kuhusu bidhaa bandia na namna ya kuzitambua jambo ambalo kwa kiasi fulani litapunguza uhalifu huo.” Amesema Erio.
Akifafanua zaidi William Erio amewaahidi ushirikiano wafanyabiashara hao katika kuimarisha ushindani sokoni na kudhibiti bidhaa bandia ili kuhakikisha walaji wanapata bidhaa zenye ubora na viwango vinavyostahili.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa udhibiti wa bidhaa bandia kutoka FCC, Godfrey Gabriel amesema wamepata mafanikio makubwa ya udhibiti wa bidhaa bandia kwa mujibu wa sheria ya mwaka 2003 na 2012, jambo ambalo limesaidia jamii kuepuka hasara na madhara ambayo yangetokea endapo wangetumia bidhaa hizo.
Katibu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo (JWK), Bw. Uroki Ombeni amewapomgeza FCC, kwa semina hiyo ambayo imewaelimisha zaidi juu ya athari za bidhaa bandia kiuchumi.
” Tutaendelea kushirikiana vyema bega kwa bega na FCC kudhibiti bidhaa bandia.Namimi nitaanzisha kampeni ya kuwasaka wale wote wanaoingiza bidhaa bandia katika Kariakoo, hatutaki ziingie kabisa,” alisisitiza.