…………………………….
Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
MKUU Wa wilaya ya Kibaha, Sara Msafiri amemuagiza ofisa mipango miji na kamati ya huduma za jamii kujipanga kutenga maeneo kwa ajili ya wafanyabiashara ndogondogo wakiwemo machinga ,wauza mitumba na wenye bidhaa za kusindika, ili kuondoa malalamiko na migogoro ambayo inajitokeza.
Aidha amewataka waliohodhi maeneo makubwa na taasisi mbalimbali pasipo kuyaendeleza wayaendeleze na wale watakaoshindwa taratibu zitachukua mkondo wake wapokonywe.
Akizungumzia katika kikao cha bajeti Cha mapendekezo ya makadirio ya mapato na matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo cha Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Mkoani Pwani, Sara alieleza , Kuna kila sababu ya kuyapangia makundi hayo maeneo yao rasmi .
“Kundi kubwa ni la vijana ,wanahangaika kujituma na shughuli ndogondogo lakini wanajikuta hawana Mazingira mazuri ya kufanya shughuli zao, ili kuepukana na haya mipango miji wekeni maeneo machinga wajulikane wako wapi, wenye bidhaa za kusindika tunazipata wapi kuliko ilivyo Sasa ,Mji huu Ni mkubwa Lazima tujipange uwe wa kisasa “alifafanua Sara.
Hata hivyo, Sara aliitaka Halmashauri ya Mji huo, kudhibiti vyanzo vya mapato na kuongeza makusanyo ili bajeti ilete matokeo.
“Rais Samia Suluhu Hassan ,anategemea kuona matokeo ya fedha za Serikali naipongeza Halmashauri hii kwa kusimamia fedha mbalimbali zinazoletwa , fedha hizi zinakuja kwa mkupuo na zinakuja kwa maelekezo ,zinahitaji usimamizi mzuri”alisema Sara.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Mshamu Munde alisema ,yapo maeneo ya wafanyabiashara ndogondogo lakini tatizo ni udhaifu wa miundombinu ya maeneo hayo na kuongeza maeneo yaliyo katika mpango.
Alibainisha kwamba , yapo maeneo Loliondo, Mailmoja na pia maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji ,Lakini Sasa wanaelekeza mipango hiyo kuitanua kwa Lengo la kuwapeleka wafanyabiashara ndogondogo pia eneo la Kidimu, mkombozi na Lumumba .
Akielezea bajeti,alisema imejielekeza kutatua changamoto za kijamii, katika huduma za afya ,sekta ya elimu na kufungua miundombinu kwenye mitaa.
Alisema ,upande wa madarasa kwasasa Kuna unafuu ,na wamepanga kuelekeza kutengeneza vyoo na madawati kwa wakati huu, na shule kongwe kuendelea kuzikarabati madarasa 26 katika shule sita .
Munde alieleza kwamba ,Kama Halmashauri imejipanga kuongeza kukusanya makusanyo zaidi ya miaka ya nyuma na kudhibiti mianya ya wizi .
Awali akisoma taarifa ya mapendekezo ya makadirio ya mapato na matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo,makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha,Selina Wilson alisema makadirio 2022-2023 inakadiria kukusanya Bilioni 45.832.4 kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato.
“Kutoka mapato ya ndani tunategemea kukusanya Bilioni 4.321.184.9 na ruzuku kutoka Serikali kuu tunategemea kupokea Bilioni 41.511.305.974.51 kati ya fefha hizi mishahara ni 31.975.459.680, matumizi mengine 0C na miradi ya maendeleo”alisema Selina.
Wakichangia bajeti hiyo, diwani wa Pangani Agustino Mdachi alisema ,bajeti ni nzuri, yenye kulenga kata zote Lakini haitoleta matokeo endapo fedha za makusanyo zitakuwa haziridhishi kwani bajeti itabaki katika makaratasi.
Mdachi alitaka ,wote Kuwa wamoja kusimamia makusanyo ya mapato kwenye vyanzo vya mapato ya ndani ili kuongeza mapato.
Nae diwani wa Tangini ,Mfalme Kabuga alieleza bajeti ipo vizuri, Lakini alimuomba nguvu kutatua changamoto ya ukosefu wa shule ya msingi na Sekondari katika kata hiyo .
Kabuga alisema ,hiyo ni kata iliyopo kwenye kitovu Cha Mji huo Lakini haina shule ya Sekondari suala ambalo linahitaji kukusimamiwa kwa maslahi ya watoto wa kata hiyo