Mkuu wa wilaya ya Mkinga Kanali Maulidi Surumbu aliyevaa kofia akimkabidhi Mche wa Mchikichi Mhandisi Modester Mushi Mkuu wa kitengo Cha Mazingira DAWASA.
…………………………
Na Lucas Raphael Tanga
Mamlaka ya Maji safi na usafi wa Mazingira mkoani Dar es salaam (DAWASA) imekabidhiwa Miche ya Michikichi 30,000 kutoka kwa Wakala wa Mbegu za kilimo (ASA) katika Shamba la Wakala Mwele mkoani Tanga.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa na Wakala wa Mbegu za kilimo ASA Mkuu wa kitengo Cha Mazingira DAWASA Mhandisi Modester Mushi alisema Miche hiyo itatumika katika kulinda na kutunza vyanzo vya maji katika Mto Ruvu.
Alisema Miche hiyo itapandwa pembezoni mwa Mto Ruvu na miche hii itatunzwa kwa kushirikiana na wananchi waishio pembezoni mwa vyanzo vya maji.
Aidha aliongeza kuwa DAWASA inatambua mpango wa serikali wa kukabiliana na changamoto ya upungufu wa mafuta ya kula Nchini ndio maana ikaamua kupanda Miche hiyo ya Michikichi kwa kuunga juhudi za serikali za kupata mafuta.
Mhandisi Modester alisema Michikichi hiyo itakuwa ni Mali ya wananchi ikiwapatia kipato kwa kupata mafuta huku ikitunza mazingira kwani ni miti yenye urafiki na mazingira.
Alisema DAWASA imejipanga kuhakikisha inakabiliana na uharibifu wa mazingira kwa kutoa Elimu kwa wananchi ikiwa na kupanda Miche hiyo ambapo itaanza kupandwa katika Mto Ruvu ambao utoa maji 92% kwa mikoa ya Dar es salaam na Pwani kutoka katika mtambo wa maji Ruvu chini uliopo Bagamoyo na Ruvu juu uliopo Mlandizi.
Alisema kwa kushirikiana na Ofisi ya Bonde la Wami/Ruvu wanatarajia kupanda vyanzo vikuu vya Maji vya Milima ya Uluguru Mkoani Morogoro ambapo ni zaidi ya kilomita 200. Kwa sasa wanatarajia kupanda Miche hiyo zaidi ya kilomita 40 kuanzia Bagamoyo katika Mtambo wa maji wa Ruvu chini.
Aliwapongeza Wakala wa Mbegu za kilimo ASA kwa kutoa Miche hiyo bure na bila kusita Mara baada ya kuomba maombi na yakajibiwa kwa haraka na hatimaye kukabidhiwa Miche hiyo 30,000.
Akikabidhi Miche hiyo Mkuu wa wilaya ya Mkinga Kanali Maulidi Surumbu aliitaka DAWASA kuhakikisha wanaitunza na kuifuatilia Miche hiyo iliiweze kutoa matokeo Kama wanayotarajia.
Alisema DAWASA wametazama Michikichi kwa jicho la tatu la kutatua changamoto ya mafuta na kuongeza Uchumi kwa wananchi kupitia mafuta watakayo kuwa wakibangua ambapo inaelezwa Michikichi huvunwa Mara nne kwa mwaka.
Mkurugenzi wa Mazao wa Wakala wa Mbegu za kilimo ASA Dkt Justine Ringo akikabidhi Miche hiyo kwa Mkuu wa wilaya ya Mkinga kabla ya kukabidhiwa kwa DAWASA alisema Wakala wa Mbegu za kilimo ASA mkakati wao nikuzalisha Miche mingi zaidi ilikutatua tatizo la Mafuta Nchini.
Aliwapongeza DAWASA kwa kuona umuhimu wa kuwa na mradi huu wa Michikichi ambayo ni rafiki wa mazingira lakini pia itasaidia kupunguza tatzo la Mafuta kwa wakazi wa maeneo hayo.
Alisema Wakala wa Mbegu za kilimo ASA Hadi Sasa imekwisha toa Miche zaidi ya 500,000 huku Uzalishaji wa Miche hiyo ukiendelea.
Dkt Ringo alizitaka Taasisi nyingine kujitokeza kuchukua Miche ya Michikichi kwa Wakala wa Mbegu za kilimo ASA ilikuunga mkono serikali kwa kukabiliana na tatizo la Mafuta.