Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kinondoni, Bw. Donassian Kessy akizungumza na waandishi wa habari leo katika Mkoa wa Dar es Salaam wakati akitoa ripoti ya miezi mitatu kuanzia mwezi Oktoba hadi Disemba mwaka 2021.
……………………………………………..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kinondoni imepokea jumla ya taarifa 133 zinazohusiana na vitendo vya rushwa katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Oktoba hadi Disemba mwaka 2021.
Imeelezwa kati ya taarifa 133 zilizohusu rushwa, wamefanikiwa kufungua majalada ambapo manne yapo katika hatua ya uchunguzi wa kina, manne yamekamilika na kwenda Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, huku 125 uchunguzi wake bado unaendelea.
Akizungumza na waandishi wa habari leo katika Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kinondoni, Bw. Donassian Kessy, amesema pia wamefungua kesi moja mpya Mahakama ya Kinondoni na kufanya jumla ya kesi zinazoendelea mahakamani kuwa 11, huku kesi mbili zimetolewa hukumu na Jamhuri imeshinda kesi zote.
Bw. Kessy amesema kuwa jukumu lao ni kuelimisha umma kupitia njia mbalimbali, lengo likiwa ni kuwasahamasisha wananchi kushiriki kwa vitendo katika mapambano dhidi ya rushwa.
Amesema kuwa wamefanikiwa kuelimisha kwa kuendesha semina 11 katika makundi mbalimbali na mikutano ya hadhara ya mitano, kushiriki onesho moja pamoja na kuimarisha klabu za wapinga rushwa 23.
Amefafanua kuwa wamekuwa na ushirikiano na taasisi mbalimbali katika kuhakikisha wanaendelea kufanya kazi kwa ufanisi ili kufikia malengo tarajiwa ya kuzuia na kupambana na rushwa.
Bw. Kessy amesema kuwa kupitia TAKUKURU inayotembea wamefanikiwa kuelimisha wananchi katika wiki ya huduma iliyojulikana kwa jina la ONE SPOT JAWABU.
Ameeleza kuwa uelimishaji huo umefanyika kwa siku saba kuanzia tarehe 16/12/2021 hadi 22/12/2021 katika eneo la viwanja vya Posta vilivyopo Kijitonyama Dar es Salaam, ulilenga kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi wa Wilaya ya Kinondoni kwa urahisi na kwa gharama nafuu katika eneo moja.
“Jumla ya taasisi 40 zilishiriki katika maonesho hayo, baadhi ni CRDB, NIDA, RITA, UHAMIAJI, NMB, DAWASCO, TRA, OSHA, TARURA, EWURA, TTCL, BRELA, CHF, NSSF, TLS NA Afisa za kazi za idara zote za halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni” amesema Bw. Kessy.
Bw. Kessy amesema kuwa wataendelea na utaratibu wa kutenga siku maalamu ya kusikiliza malalamiko na kero za wananchi kwa kutenga siku maalumu ya kusikiliza malalamiko na kero za wananchi kwa kuwafata maeneo mbalimbali chini ya mpango wa TAKUKURU inayoendelea.
Ametoa wito kwa wananchi wote kuendelea kutoa ushirikiano pamoja na kuepuka matapeli wanaoibuka na kuwapigia simu wananchi kwa kujifanya wao ni maafisa wa TAKUKURU, huku wakiwatapeli kuwatishia kuwa wana tuhuma zao hivyo kuwadai pesa wawasaidie kufuta huhuma hizo.