Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango akizungumza na wachezaji na viongozi wa timu ya taifa ya wanawake chini ya umri wa miaka 20 ( Tanzanite) wakati alipoitembelea timu hiyo katika Ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia jana tarehe 04 Februari 2022.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango akiwa katika picha ya pamoja na wachezaji na viongozi wa timu ya taifa ya wanawake chini ya umri wa miaka 20 ( Tanzanite) wakati alipoitembelea timu hiyo katika Ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia jana tarehe 04 Februari 2022.
……………………….
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango jana tarehe 04 Februari 2022 akiwa nchini Ethiopia, amewatembelea na kufanya mazungumzo na wachezaji na viongozi wa timu ya taifa ya wanawake chini ya umri wa miaka 20(Tanzanite) mazungumzo yaliofanyika katika ubalozi wa Tanzania Nchini Ethiopia.
Makamu wa Rais amewapongeza wachezaji hao na viongozi wao kwa hatua waliofikia pamoja na kupeperusha vema bendera ya Tanzania katika mashindano mbalimbali wanayoshiriki. Amesema siku zote timu hiyo ya wanawake imekuwa ikitangaza vema jina la Tanzania katika michezo.
Aidha Makamu wa Rais amewaasa Makocha na Viongozi wa timu hiyo kuwalea vema wachezaji hao ili waendelee kuwa na mchango katika taifa. Makamu wa Rais amesema michezo ni afya na ajira hivyo itawawezesha wachezaji hao kuendelea kupata kipato.
Aidha amewatakia heri wachezaji hao katika mechi yao dhidi ya Ethiopia na kuwaeleza kwamba Watanzania wote wapo pamoja na timu hiyo na kuwaombea kupata matokeo mazuri.
Timu ya taifa ya Tanzania ya wanawake chini ya miaka 20 ipo nchini Ethiopia kucheza mchezo wa pili wa kutafuta tiketi ya kushiriki fainali za kombe la dunia kwa wanawake nchini Costa Rica baadaye mwaka huu.
Makamu wa Rais yupo nchini Ethiopia kumuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa 35 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) unaotarajiwa kufanyika tarehe 5 na 6 Februari 2022.