Na Sixmund Begashe
Vijana na wananchi mbalimbali nchini wameshauriwa kwenda Makumbusho ya Azimio la Arusha kujifunza misingi muhimu iliyowekwa na waasisi wa nchi hii wakiongozwa na Hayati Baba wa Taifa Mwl Julia Nyerere 1967.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Makumbusho ya Azimio la Arusha Dkt Gwakisa Kamatula kwenye Maadhimisho ya miaka 55 ya Azimio la Arusha yanayoendelea katika Viwanja vya Makumbusho hiyo iliyopo Jijini Arusha.
Dkt Kamatula amesema kuwa wameamua kuanzisha maadhimisho hayo ili kupanua wigo wa kutoa elimu na kuirithisha jamii urithi adhimu wa Azimio la Arusha hasa kwa kizazi cha sasa ambacho hakina uwelewa mpana kuhusu misingi imara ya nchi iliyosimikwa kupitia Azimio hilo.
” Waasisi wa Taifa letu chini ya Hayati Baba wa Taifa Mwl Julius Nyerere, baada ya Uhuru walikutana Arusha na kuweka misingi imara iliyosaidia na inaendelea kusaidia kusukuma maendeleo ya nchi misingi hiyo ni kama vile Umoja wa Kitaifa, Uwajibikaji, Udugu na Umoja, Utu, Uchapaji kazi kwa faida ya wote nk” Dkt Kamatula
Naye Mratibu masaidizi wa Maadhimisho hayo Bi Elizabeth Solomoni amesema maadhimisho ya Mwaka huu yamehusisha Mada na Maonesho ya Vitu halisia vilivyotumika katika Mkutano wa Azimio, Majadiliano, wajasiriamali na burudani ya sanaa mbalimbali.
Wakazi mbalimbali waliotembelea kwenye Maadhimisho hayo akiwepo Bw Juma Kombo mkazi wa Babati wameipongeza Makumbusho ya Taifa kupitia kituo cha Makumbusho ya Azimio la Arusha kwa hatua iliyoichukuwa ya kuanzisha Tamasha la Azimio la Arusha kwani kupitia Tamasha hilo watu wengi watakuwa na hufahamu mkubwa wa umuhimu wa kuishi katika misingi ya Azimio hilo.
” Watoto wetu wengi hawana ufahamu kabisa juu ya Misingi iliyowekwa katika Azimio hili, wamekuwa wakifuata misingi ya nchi zingine, wengi wamejaa ubinafsi, wengine wanawauwa hadi wazazi wao hawana Utu, heshma imepungua, lakini kwa njia hii hakika sisi wazazi tunapata matumaini’ Mzee Juma Kombo
Tamasha limeanza tarehe 1 Feb 2022. na litafungwa na kuzindua miradi ya ustawi wa taifa na mapambano dhidi ya UVIKO 19 inayotekelezwa katika vituo vya Azimio la Arusha na Elimu viumbe, Jijini Arusha.