Na Said Mwishehe, Michuzi TV
MWENZENU sijui nimeumbwaje kuna wakati huwa najipa kazi za kufanya ambazo ukiniuliza lengo langu ni nini huwa nakosa majibu, ndio nitajibu nini sasa? Usinicheke niko siriasi.
Leo nimeamua kujipa kazi ya kufanya, Ndio. Nimekaa wee nikaona mbona nipo nipo tu,lakini wakati naendelea kutafakari kuhusu maisha kichwani yakaanza kupita mambo mengi mengi, basi ndio hivyo ,sasa unafikiria kwa Januari hii nitatoa wapi ya maana sana.
Eti nikaanza kutafakari yanayofanywa na viongozi wetu wa ngazi mbalimbali, nikawa najaribu kuwapima wanayofanya na kutenda kwa ajili ya Watanzania, yaani ngoja nikwambie unayesoma haya maandishi yangu,nimewachambua viongozi balaa utadhani kuna malipo nitapewa kumbe wapi.Siunajua ule msemo unaosema ukikosa kazi Shetani atakutafutia kazi.
Sawa huo ndio msemo wa Wahenga lakini hii kazi niliyojipa haina uhusiano na ukikosa kazi basi Shetani anakutafutia kazi ya kufanya. Nimejipa mwenyewe, nafahamu viongozi wapo wa kada tofauti lakini nimeamua kujikita kwa wakuu wa Wilaya, hawa ni viongozi muhimu kwani wako karibu zaidi na wananchi. Wakuu wa Wilaya ndio wawakilishi wa Rais kwa ngazi ya Wilaya.Uwepo wao ni muhimu.
Hivyo hata kujipa kazi ya kuwatafakari kuhusu utekelezaji wao wa majukumu naona sio jambo baya. Kwanza nikiri wakuu wa Wilaya ambao wameaminiwa na Rais wengi wanafanya kazi kubwa na nzuri,wanastahili pongezi,nami nawapongeza wakuu wa Wilaya wote nchini .
Wakati naendelea kutafakari kazi zinazofanywa na wakuu wa Wilaya kichwani kwangu likanijia jina la Jokate Mwegelo, Ni Mkuu wa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam, kabla ya kuwaTemeke alikuwa Wilaya ya Kisarawe.
Akiwa Kisarawe ndipo nilipoamua kujipa muda wangu mwingi kumfutilia utendaji wake na staili yake anayotumia katika kuwatumikia wananchi kwa ngazi ya Ukuu wa Wilaya.Ngoja nikwambie mtu wangu Jokate ni kiongozi anayejua nini anatakiwa kufanya kwa ajili ya wananchi anaowatumikia.
Hivyo pamoja na kufuatilia utendaji kazi wa wakuu wa Wilaya katika maeneo mbalimbali naomba nijikite kwa Jokate,kwangu huyu ni Mkuu wa Wilaya wa mfano, ni kijana wa kitanzania mwenye maono makubwa ya kulitumikia Taifa lake.
Kauli na matendo yake yanathibitisha ninayo yasema .Jokate ni miongoni mwa Wakuu wa Wilaya ambao wanaamini katika kusimamia na kuyatekeleza anayoyasema.
Kwa Kisarawe Jokate ameacha kumbukumbu ambazo zitakumbukwa na vizazi vya sasa na vijavyo,alifanya hivyo kwa mapenzi yake mema kwa kwa Wananchi lakini kwa mapenzi yake makubwa kwa Taifa lake.Kwa akili zangu za kijinga kuna wakati natamani tungekuwa na akina Jokate wengiiii lakini hiyo haiwezekani,
Mungu amempa kila kiongozi karama za kuongoza kwa staili yake.Hongera Jokate, Mungu amekupa upendeleo kwa kukujaza wingi wa busara na maarifa, unajua kuzitumia tena ukijumlisha na elimu yako ndio kabisa, yaani hadi raha.Hongera ndugu best.
Nafahamu Kisarawe Jokate alikwenda kuwa Mkuu wa Wilaya baada ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.John Magufuli( ametangulia mbele za haki) kuamua kumteua kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe.Hakika Dk.Magufuli alifanya uamuzi sahihi,Jokate amefanya makubwa Kisarawe.Kama huamini kawaulize Wana Kiarawe watakwambia .
Amefanya mengi ya Maendeleo ya wananchi lakini pia hakubakia nyuma katika sekta ya utalii,ameipigia debe kwa kiwango kikubwa .Ni Jokate aliyekaa na kuamua kuja na wazo la kuanzisha Tamasha la Utalii Kisarawe ambalo lilipewa jina la Ushoroba Kisarawe Festival.
Ni Tamasha ambalo limekwenda kuhamasisha utalii wa Wilaya ya Kisarawe.Limebakia kama kumbukumbu kwa Wana Kisarawe.Akaifanya Hifadhi ya Msitu ya Mazingira Asilia Pugu Kazimzumbwi kujulikana kila kona ya nchi yetu, watalii wakaongezeka.
Takwimu za Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania( TFS) Kanda ya Mashariki na Pwani ziko wazi na wanakiri Jokate amefanya kazi kubwa katika kuutangaza utalii.Ndio wakati wake Dunia ikajua kumbe pazi mwenye rangi ya bendera ya Tanzania anapatikana Pugu Kazimzumbwi.Ukipata nafasi nenda utamuona.
Mkuu wa Wilaya wa aina hii (Jokate)anastahili kutambuliwa na kupewa heshima japo ya kusema tu kile ambacho amekifanya.Ni mengi ya kuzungumzia yaliyofanywa na Jokate,hakuna aliyesahau kampeni yake ya kupigania ujenzi wa barabara inayopita katika mji wa Kisarawe kuelekea Hifadhi ya Selue wilayani Rufiji.
Leo hii barabara hiyo iko kwenye mipango ya serikali na ujenzi unafanya kuhakikisha inapitika vizuri,alioombea na lami, ila sijafuatilia ,ukimaliza kusoma nenda kafuatilie.Ndio,unakunja sura ili iweje?
Kwangu namuona Jokate kama kiongozi kijana ambaye akiendelea na staili yake hii ya uongozi atafika mbali zaidi ya alipo sasa.Kama nilivyoeleza awali Jokate alianzia Kisarawe lakini mama yetu,Rais Samia Suluhu Hassan amempeleka Wilaya ya Temeke, nako ameanza vizuri
Anayoyafanya Temeke yanastahili kila aina ya pongezi.Jokate anajua kupambana sana,anajua kusimamia makumu yake.Temeke wameanza kufurahia yanayofanywa na Jokate, acha utani huyu dada anajua kuongoza.Hongera mwaya!
Hongera Mkuu wa Wilaya Jokate Mwegelo, wenyewe zamani walikuzoea kwa jina la Kidoti,ndugu yangu unaupiga mwingi.Temeke nasikia kuna kitu umekianzisha kinaitwa Temeke Gulio ,lengo kuwawezesha wajasiriamali kufanya biashara zao bila vikwazo.Nakukubali sana.
Maagizo na maelekezo yako yamekuwa funguo ya kufanikisha mipango ya maendeleo kama Rais wetu anavyotaka Tanzania iwe.Ahsante Rais Samia kwa kuendelea kumuamini Jokate.Anakuwakilisha vizuri.
Jokate ngoja nikwambie endelea kuwatumikia wananchi wa Wilaya ya Temeke,najua uwezo wako,najua umakini wako, sifa yako ya kuwasikiliza wananchi na kutatua changamoto zao nikuombe endelea kuifanya na Temeke,Rais Samia amekuamini na Wana Temeke Wana imani na wewe.Piga kazi,songa mbele.
Tunajua namna ambavyo wanawake wakipewa nafasi za uongozi huwa hawashindwi, wanajua kutumikia kwa uadilifu na uaminifu dhidi ya wale wanaowaongoza.Kinachofurahisha kwa Jokate umethibitisha vijana wa Tanzania wakiaminiwa wanaweza.
Kuna wakuu wa Wilaya wengi vijana wanafanya vizuri, leo tu nimeamua kumzungumzia Kidoti.Kisarawe wenyewe walikuwa wanamuita Kihindi Kideke yaani Hindi changa kwa lugha nyepesi kabisa kabinti kadogo.
Kwa kuwa nimeamua kumzungumzia Jokate na utendaji wake,ngoja nikwambie hivi Jokate aliyezaliwa Machi 20 mwaka 1987 amepita katika hatua mbalimbali kama ambavyo wanapitia wengine, kama Kuna tofauti basi inaweza kuwa ndogo sana.
Kwa mfano tunajua vijana wote wamezaliwa kwa hiyo tofauti itakuwa umezaliwa wapi,Jokate kazaliwa katika Jiji la Washington DC nchini Marekani,ndio ujue hivyo, unashtuka nini?Jokate uzuri wake hana maringo,hana majivuno.Huwezi kujua hadi uambiwe.Kwanza hapendi sifa za kijinga.
Ukiondoa kuzaliwa Marekani Jokate huko nyuma amewahi kuwa muigizaji wa filamu ,kazi iliyompatia umaarufu,Jokate ni mjasiriamali na mwanasiasa kutoka nchini Tanzania.Amepita njia mbalimbali za kusaka maendeleo hadi pale Julai 2018 alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya.
Jokate amewahi kuwa mtangazaji na mwimbaji lakini kubwa zaidi amewahi kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Kidoti Company.Hata hivyo niweke vizuri kidogo nimesema amezaliwa Marekani lakini hiyo ilitokana na mmoja ya wazazi wake kufanya kazi katika nchi hiyo ,hivyo katika kukua kwake amekulia katika Jiji la Dar es Salaam.
Na alianza elimu ya msingi katika shule ya Olympio Primary School na baadaye St. Anthony High School, halafu Loyola High School, Dar es Salaam.
Aliipenda elimu na elimu ikampenda kwani baada ya kusoma Loyola High School alifaulu na kisha akajiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo alipata Shahada ya Sayansi ya Siasa na Falsafa.Jokate aina ya uongozi ni uongozi wa tuzungumze,tusikilizane,tuelewane na kisha tuamue, lakini hii ni kwa mtazamo wangu.
Mbali na hayo niwe mkweli Jokate pamoja na yote ana sifa zote za uzuri,Mungu alijua kumuumba, alijua kumtengeneza. Anakidoti cheusi na vidimpo kwa mbali, utatamani kumuangalia muda wote,kha ! Jamani! Unashangaa nini ,ngoja nikwambie huenda umesahau Jokate amewahi kuwa Mshindi wa pili katika Shindano la Miss Tanzania, ilikuwa mwaka 2006. Katika shindano hilo Wema Sepetu aliyeshika nafasi ya kwanza .
Nakumbuka ushindani ulikuwa mkubwa sana.Wema Sepetu sauti yake laini ilimpa kete ya Ushindi, tofauti ilikuwa moja siku hiyo Jokate alikuwa vizuri kichwani, Wema Sepetu alikuwa vizuri mdomoni.Jokate vilevile alipewa jina la balozi wa Redds fashion na balozi wa gazeti la Citizen, baada ya kupata kura nyingi mwaka huo.
Kabla ya Miss Tanzania, alishindana katika Miss Kurasini 2006, shindano ambalo alishinda, kisha kuelekea juu zaidi na kuwa Miss Temeke 2006, ambako pia alishinda
Kuhusu maisha yake ya Kazi Mwaka 2018 ateuliwa na Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe. Na katika kuigiza mwaka wa 2007, alipata kucheza filamu yake ya kwanza iliyojulikana kwa jina la Fake Pastors, akiwa na Vincent Kigosi, Lisa Jensen, mshindi wa tatu wa Miss Tanzania 2006 na marehemu Adam Kuambiana.
Mwaka wa 2008, akacheza katika filamu ya From China With True Love na mwaka 2010, alionekana katika filamu ya Chumo, filamu iliyoandaliwa na Media for Development International, kuhusu elimu juu ya ugonjwa wa malaria.
Filamu hiyo ilimwezesha kupata tuzo ya Zanzibar International Film Festival akiwa kama mwigizaji bora wa kike kwa 2011 na kuchaguliwa kama mwigizaji wa Pan-Afrika katika tuzo za 2012 Nigeria Entertainment Awards.
Vilevile amepata kuonekana katika mfululizo wa TV maarufu wa Siri Ya Mtungi, uliokuwa unaandaliwa na Jordan Riber na kuongozwa na Karabani, mnamo 2013.Mwaka wa 2014, amecheza uhusika wa “Ndekwa” katika filamu ya Mikono Salama, ambayo ilimpelekea apate tuzo nyingine ya Zanzibar International Film Festival akiwa mwigizaji bora wa kike kwa filamu za Kiswahili.
Pia amewahi kushirikishwa katika wimbo wa Japo Nafasi wa Cpwaa akiwa na A.Y. katika wimbo wa Kings and Queen, na Amani, kutoka Kenya. Mwaka wa 2013, alitoa wimbo wake akiwa na Lucci, uliyoitwa ‘Kaka na Dada.Wakati Mwaka wa 2015, akadondosha wimbo wake mwingine uliyoitwa Leo akiwa na mwimbaji mwingine kutoka nchini Nigeria maarufu kama Ice Prince.
Kwenye siasa Jokate hakujulikana kujishughulisha na siasa hadi mwaka 2017 alipoteuliwa na Umoja wa Vijana wa chama cha CCM (UVCCM) kuongoza Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi ya umoja huu akiwa kaimu katibu wa idara hii.
Yeye mwenyewe alitaja maarifa ya utoto wake alipohamasishwa na bibi yake aliyekuwa mwasisi wa Umoja wa Walimu Tanzania katika Mkoa wa Rukwa kuona ni muhimu kujitoa katika jamii na kuchukua nafasi za uongozi.Wakati ule magazeti yalileta taarifa kuwa uteuzi wake ulipingwa na sehemu ya viongozi wa umoja huu.
Nihitimishe kwa kusema tu nakushuru kwa kusoma maandishi haya kuanzia mwanzo hadi mwisho, ahsante kwa kunielewa na pale ambapo nimekuchanganya kidogo tuvumiliane ,tuombe uhai bado tunayo nafasi ya kuendelea kujuzana.Lakini kubwa na la msingi nimeandika nikiwa na akili zangu timamu,sijashawishiwa wala kulazamishwa na mtu.
Kwa Mkuu wa Wilaya ya Temeke Jokate Mwegelo nisamehe ,kwani nimeamua kukuzungumzia kwa jinsi ninavyokufahamu bila ridhaa yako.Nilipokosea basi nisamehe na kama hakuna la maaana ambalo nimelisema kuhusu wewe naomba ushike japo hili tu ya kwamba unaitendekea haki nafasi ya Ukuu wa Wilaya .Piga kazi,uko kazini na bahati nzuri Rais wetu Samia naye yuko kazini.Hivyo kazi iendelee.
Simu yangu 0713833822