Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi Paskas Mulagiri kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk.Binilith Mahenge akipanda mche wa mti wakati akizindua zoezi la upandaji miti Mkoa wa Singida lililofanyia eneo la Maziwa ya Kindai na Munang Manispaa ya Singida lililoratibiwa na Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Trees for the Future Tanzania ambapo miche ya miti 2000 ilipandwa.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Singida Yagi Kiaratu akishiriki kupanda miche ya miti katika eneo hilo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida, Zefrin Lubuva akizungumza wakati wa zoezi hilo la upandaji wa miche ya miti.
Kaimu Mkuu wa Idara Mazingira Manispaa ya Singida Shuku Kaishwa akitoa taarifa ya zoezi hilo la upandaji wa miche ya miti.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Stella Mutahibirwa akishiriki kupanda miche ya miti.
Maafisa kutoka Bodi ya Maji Bonde la Kati wakishiriki zoezi la kupanda miche ya miti. Kutoka kulia ni Mhandisi Moses Silungu na Kaimu Afisa Maji Bodi ya Maji Bonde la Kati, Danford Samson.
Kaimu Afisa Maji Bodi ya Maji Bonde la Kati, Danford Samson (katikati) akishiriki kupanda mche wa mti. Wengine ni maofisa kutoka Bodi ya Maji Bonde la Kati.
Baadhi ya Wafanyakazi wa Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Trees for the Future Tanzania wakiwa kwenye zoezi hilo.
Na Dotto Mwaibale, Singida
MKUU wa Mkoa Singida Dk. Binilith Mahenge ameiagiza Manispaa ya Singida kuhakikisha inawakamata watu wote watakaoacha mifugo yao ikizurura hovyo na kusababisha uharibifu wa mazingira kwa namna yoyote ile.
Agizo hilo limetolewa mkoani hapa leo wakati wa uzinduzi wa zoezi la upandaji miti kimkoa lililofanyika eneo la maziwa ya Kindai na Munang lililoratibiwa na Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Trees for the Future Tanzania lenye lengo la kuhimiza watanzania kuongeza juhudi katika shughuli za uhifadhi wa mazingira
Kupitia kampeni hiyo na kwa muktadha wa kufanikisha lengo la kitaifa-kila Halmashauri ikiwepo Halmashauri ya Manispaa ya Singida imeagizwa kupanda miti isiyopungua milioni 1.5 ili kufanikisha lengo la ukijani na utunzaji thabiti wa rasilimali misitu kwa kila halmashauri husika.
” Ninaagiza mazingira yatunzwe na mifugo isiruhusiwe kuzurura hovyo-hivyo naagizawekeni utaratibu mzuri na muwe na tabia ya kupanda miti na kuitunza ili iwe endelevu kwa kizazi cha sasa na baadae” alisema Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi Paskas Muragili kwa niaba ya mkuu wa mkoa”
Katika hatua nyingine Dk. Mahenge ameagiza kila kaya mkoani hapa kuhakikisha inalima ekari isiyo pungua moja ya zao la mtama aina ya serena ili kukabiliana na uhaba wa chakula ambao utaweza kutokea kutokana na changamoto zilizopo za mabadiliko ya hali ya hewa.
Hata hivyo kwa muongozo wa kauli mbiu ya uzinduzi huo isemayo ‘Miti, Mazingira Yangu, Tanzania Yangu’- Msimamizi wa miradi wa Taasisi hiyo Veliksi Haji alisema shabaha ya taasisi hiyo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ambayo pamoja na mambo mengine inajihusisha na uhamasishaji wa kilimo endelevu kwa kutumia miti wameazimia kupanda takribani idadi ya zaidi ya miti milioni tatu ambayo ina uwezo wa kustahimili hali ya hewa ya eneo husika.
Kwa upande mwingine, Wizara ya Maji kupitia ofisi yake ya Bodi ya Maji Bonde la Kati ambayo imepewa dhamana ya kutunza vyanzo vya maji ikiwemo maziwa hayo imetahadharisha wananchi kuendelea kuchukua hatua za uhifadhi wa vyanzo vyote vya maji na kuvilinda ipasavyo ili kupendezesha mji, kuweka mandhari nzuri, kuzuia mmomonyoko wa ardhi na kuthibiti kuenea kwa jangwa ambako kunaweza kupelekea kupungua kwa vina vya maji.
Kaimu Afisa wa Maji Bodi ya Maji Bonde la Kati, Danford Samson kwa niaba ya wizara alitoa angalizo hilo wakati wa kampeni hiyo ikiwa ni sehemu ya jitihada ya ofisi hiyo kuhakikisha kampeni ya kufanya Singida kuwa kijani inafanikiwa.