Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mh. Nape Nnauye amefanya ziara ndani ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL – Corporation) na kubainisha kuwa lengo la wizara yake ni kuifanya taasisi hiyo kuwa kitovu cha mawasiliano kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Waziri Nnauye amebainisha hayo leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya kutembelea TTCL – Corporation na kuzungumza na menejimenti ya shirika pamoja na kupokea taarifa na changamoto zinazolikabili shirika.
“Tageti yetu ni kuifanya TTCL – Corporation kuwa shirika bora la mawasiliano kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, Tunataka tutafute njia ya pamoja ya kuliboresha shirika hili,” alisema Waziri huyo wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mh. Nnauye akizungumza na wanahabari.
Alisema katika ziara hiyo aliyoiita ya kujifunza wamepokea taarifa ambapo, yapo mambo yaliyowasilishwa kama changamoto ambayo yanakwamisha shirika hilo kufanya vizuri zaidi, hivyo kama wizara inayoisimamia inakwenda kukaa na kuyachakata kabla ya kuyatolea maelekezo.
“Tumeyapokea na tunaenda kukaa na kuyachakata, yanayopaswa kufikishwa mamlaka za juu tutayawasilisha na yaliyochini yetu tunaenda kuyafanyia kazi kisha baadaye tutatoa maelekezo yetu ili kusonga mbele,” alifafanua waziri huyo.
“…Alitolea mfano kuwa zipo sheria za manunuzi ya umma ambazo TTCL imekuwa ikilazimika kuzifuata mchakato wake unaweza kuchukua hadi miezi sita, wakati sekta binafsi ambao ni washindani wa TTCL unaweza hata kuchukua siku mbili…sasa ukimwacha hapo kushindana na wenzake lazima ataachwa mbali,” alisema Waziri Nnauye.
Aidha akifafanua zaidi alisema yapo baadhi ya mambo ya kimaamuzi ambayo TTCL haiwezi kufanya pekee hadi kushirikisha ngazi nyingine, jambo ambalo limekuwa kama changamoto kwenye shirika na kukwamisha baadhi ya mipango ya maendeleo ya shirika.
Aliongeza kuwa wamejipanga kukutana pia na wafanyakazi wa TTCL na kuzungumza nao ili kupata maoni na changamoto zao na kuangalia namna bora ya kushirikiana kuhakikisha shirika linasonga mbele kwa mafanikio zaidi.