Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania TANESCO Maharage Chande akizungumza Leo Januari 24, 2022 Jijini Mwanza wakati akifungua kikao kazi cha mameneja na wasimamizi wa vituo vya usambazaji umeme kutoka Mikoa ya Tanzania Bara.
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeweka mkakati wa kupima utendaji kazi wafanyakazi kuwa miongoni mwa vigezo za vya motisha kwa wafanyakazi wanaofanya vizuri katika jitihada zinazoendelea za kuboresha utoaji wa huduma kwa wateja.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji, Maharage Chande Januari 24, 2022 Jijini Mwanza wakati akifungua kikao kazi cha mameneja na wasimamizi wa vituo vya usambazaji umeme kutoka Mikoa ya Tanzania Bara.
“Kupitia kipimo hiki, wafanyakazi wote watakaotimiza vyema majukumu yao tutawapatia motisha na wale watakaoshindwa kufikia malengo tutawasaidia ili nao waweze kulisaidia Shirika kutimiza malengo yake” alisema Maharage.
Kwa upande wake Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji Usafirishaji Umeme, Mhandisi Abubakary Issa amesema pamoja na mambo mengine, kikao kazi hicho kinalenga kujadili na kuandaa mpango kazi utakaochochea ufanisi katika utendaji wa shirika chini ya kaulimbiu isemayo “timu yenye ufanisi kwa ufanisi wa gridi”.
Meneja Mwandamizi Kanda ya Ziwa, Mhandisi Henryfried Byabato amesema kikao kazi hicho kitakuwa na manufaa makubwa kwa Shirika hususani katika kusaidia kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme kwenye gridi kuimarika.
Katika hatua nyingine Maharage amefafanua kwa sasa uzalishaji wa umeme nchini ni zaidi ya megawati 1,600 ambazo hata hivyo bado hazitoshelezi mahitaji halisi ya nchi hivyo kukamilika kwa miradi ya kimkakati kama mradi wa bwawa la kufua umeme wa maji la Julius Nyerere (JNHPP) utawezesha TANESCO kuzalisha megawati 2115 ambazo zitasaidia umeme kuwa wa uhakika, unaotabirika.
“Nchi yoyote duniani, maendeleo yake yanategemea nishati ya umeme hivyo ninyi mmebeba mzigo mkubwa wa kufanya Taifa liendelee ama kubaki lilipo. Uwezo wenu wa kuhakikisha tuko imara ndio utasababisha tusonge mbele” alisema Maharage.
Katika hatua nyingine ameongeza kuwa shirika linaendelea na juhudi za kutatua changamoto mbalimbali zikiwemo uhaba wa vitendea kazi vya kisasa, magari pamoja na kutoa mafunzo kwa wataalamu wake ili kuhakikisha wanafanya kazi kwa weledi hususani kuboresha mifumo ya mashine kujiendesha (automation) katika vituo vya kusukumia umeme.