……………………………………………………..
Na Angela Msimbira, NJOMBE
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe Innocent Bashungwa amemuagiza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara vijijini na Mijini (TARURA) Mhandisi Victor Seff kuandika taarifa ya kina inayoonyesha changamoto wanazokabiliana nazo katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo.
Ameyasema hayo akiwa ziarani mkoani Njombe kukagua miradi ya maendeleo ikiwemo miundombinu ya barabara, elimu na afya.
Waziri Bashungwa amesema kuwa bado kuna mdororo wa utekelezaji wa maamuzi, usimamizi mbovu wa utekelezaji wa majukumu katika ngazi za Mikoa na Halmashauri na anahitaji kuona TARURA ambayo inawajibika kwa wananchi.
Ameiagiza TARURA kuhakikisha mchakato wa manunuzi unafanyika mwanzoni mwa mwaka wa fedha ili vifaa viweze kufika kwa wakati na kazi kuanza bila kuchelewa na kuhakikisha mwaka wa fedha unapoanza kazi ya usanifu inaanza mapema ili fedha inapoingia kazi ianze.
Pia, ameelekeza wasanifu wa miradi wabobezi watoke makao makuu na kwenda kusanifu miradi kwenye wilaya na mikoa na kama kuna upungufu wa watumishi waangalie namna bora ya kuajiri watumishi kwa mikataba ili waweze kusaidia katika kusanifu miradi.
Mhe. Waziri ameitaka TARURA kuhakikisha wanatoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa ujenzi miradi kwa viongozi wa Halmashauri hasa madiwani na si kusubiri bodi ya barabara ya Mkoa na kuelekeza kuwa kila kwenye baraza la madiwani Meneja wa Wilaya lazima ashiriki vikao hivyo ili kujibu hoja zinazojitokeza katika masuala ya barabara.
Pia, ameelekeza kupatiwa taarifa ya kila mwezi ya utendaji kazi wa Mameneja wa Mikoa ili kubaini wazembe na wachapakazi ili kwa wale wazembe watakaoshindwa kutimiza majukumu yao wachukuliwe hatua.
Aidha, amesema fedha zinazoingia TARURA zisizidi siku tatu ziwe zimekwenda kwenye Wilaya husika kwa ajili kuanza kazi utekelezaji wa miradi.