Baadhi ya Mahakimu na Majaji wa Chama cha Mahakimu na Majaji Wanawake Tanzania Kanda ya Songea wakishiriki matembezi ya km4 wakati wa Uzinduzi wa Maadhimisho ya wiki ya utoaji elimu ya sheria,ya wiki ya Utoaji elimu ya Sheria mkoani Ruvuma.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Songea Sekela Moshi katikati akiongoza matembezi kwa watumishi wa Mahakama na wadau wa sheria wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya utoaji elimu ya sheria kwa wananchi wa mkoa wa Ruvuma, kulia Katibu Tawala wa mkoa wa Ruvuma Stephen Ndaki na kushoto Kaimu Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dkt Julius Ningu.
Waendesha Boda boda katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wakishiriki matembezi wakati wa Uzinduzi wa wiki ya sheria kanda ya Songea inayoendelea katika viwanja vya Soko Kuu mjini Songea
Baadhi ya watumishi wa Mahakama kanda ya Songea na wadau mbalimbali wa sheria wakiwa katika matembezi yaliyolenga kuhamasisha wananchi kwenda kupata elimu na ushauri wa kisheria inayotolewa katika Mahakama ya Tanzania wakati wakati ya uzinduzi wa Maadhimisho ya wiki ya utoaji elimu ya sheria.
………………………
Na Muhidin Amri, Songea
UZINDUZI wa Maadhimisho ya wiki ya utoaji wa Elimu ya Sheria kanda ya Songea, umefanyika kwa watumishi wa Mahakama na wadau wa sheria kufanya matembezi umbali wa km 4 kama sehemu ya kuhamasisha jamii kufahamu kazi mbalimbali za mahakama na kwenda kupata elimu na ushauri wa kisheria.
JAJI Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Songea Sekela Moshi alisema, katika wiki ya sheria Mahakama na wadau mbalimbali ikiwamo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali,Tume ya Haki ya Binadamu na utawala Bora hujumuika na kutoa elimu na ushauri wa kisheria kwa wananchi bila malipo.
Alisema, Maadhimisho ya haya na kilele cha siku ya sheria nchini huashiria kuanza kwa mwaka mpya wa kimahakama ambao ni mwanzo wa shughuli katika mwaka ambayo uambatana na maonesho mbalimbali yaliyofanyika toka kuanzishwa rasmi kwa Mahakama Kuu Tanzania mwaka 1920.
Jaji Moshi alisema,Watumishi wa Mahakama wakiwamo Mahakimu,Majaji na wadau watatoa ushauri na elimu ya kisheria chini ya Kauli Mbiu ‘Zama za Mapinduzi ya nne ya Viwanda,Safari ya Maboresho kuelekea Mahakama Mtandao’ kwa kuwa Mahakama ndiyo chombo pekee chenye mamlaka ya kutoa haki.
Alisema,ni ukweli usiopingika kuwa katika zama hizi za Mapinduzi ya nne ya viwanda matumizi ya Tehama hayaepukiki katika shughuli za utoaji haki wanapoelekea Mahakama Mtandao ambapo Tehema imechukua sehemu kubwa katika Mapinduzi ya viwanda ambayo ndiyo inayoendesha uchumi wa nchi.
Alisema, unapozungumzia maboresho na kuifikisha mahakama katika hadhi itakayotoa haki kwa njia ya mtandao ambapo watumishi,wadau na wananchi kwa jumla lazima wawe sehemu ya mapinduzi hayo.
Kwa mujibu wa Jaji Moshi, katika zama hizi za nne za mapinduzi ya viwanda mahakama imepiga hatua kubwa hasa juu ya matumizi ya Tehama katika kuendesha shughuli zake kwa njia ya mtandao ikiwamo kufungua mashauri,usikilizwaji wa mashauri(kwa video conference)utunzaji kumbukumbu na utoaji nyaraka mbalimbali.
Hata hivyo alisema, hayo hayataweza kufanikiwa kama wadau na wananchi hawatakuwa na tabia ya kujisomea kama ilivyo lengo la nne la Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2025 ambapo Serikali inasisitiza umuhimu wa kuwa na Taifa la watu wanaopenda kujisomea.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge alisema, Serikali kama mdau muhimu wa mahakama ya Tanzania ina tambua mchango mkubwa unaotolewa na mahakama katika kujenga nchi inayozingatia Uhuru,haki,udugu,Amani na ustawi wa jamii.
Brigedia Jenerali Ibuge ambaye katika uzinduzi huo aliwakilishwa na Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Dkt Julius Ningu alisema,kadri mahakama inavyozidi kufanya maboresho ya utoaji huduma zake kwa kujikita zaidi katika matumizi ya Tehama.
Ibuge alisema, ni ukweli kwamba matumizi ya Tehama yanasogeza huduma karibu kwa wananchi na inarahisisha upatikanaji wa taarifa kwa wadau na wananchi.
Mkuu wa mkoa,ameipongeza Mahakama nchini kwa kuboresha huduma zake na kutolea mfano ujenzi wa vituo vya utoaji haki na ukarabati wa majengo yake ili kuendana na mapinduzi ya nne ya viwanda na usikilizwaji mashauri kwa njia ya mtandao.
Alisema,katika maboresho hayo yanayoendelea kufanyika kwa mkoa wa Ruvuma, Mahakama kuu kanda ya Songea iko kwenye harakati za kusogeza huduma karibu kwa kujenga jengo la kisasa wilayani Namtumbo na mahakama ya mwanzo Matiri wilaya ya Mbinga.