“Watangaza nia uchaguzi ndani ya chama umepita ni kuunga mkono kwa mteuliwa” Kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) aliyetangaza nia ya Kugombea nafasi ya Spika wa bunge Mkurugenzi Mtendaji wa Msama Promotions Alex Msama amesema kuwa wanawake wanauwezo mkubwa wa kuongoza hivyo wanaume tutulie.
Msama ameyasema leo Januari 22 mwaka huu mara baada ya kutangazwa kwa Mgombea Uspika kwa tiketi ya chama hicho Dk.Tulia Ackson Mwansasu ,amesema kuwa wakati wanaume wamekuwa katika nafasi za juu wanawake hawakusema chochote hivyo ni wakati wao umefika kuonyesha uwezo wao.
Msama amesema kuwa Dk.Tulia ana uwezo kwa nafasi hiyo na matokeo yake yataonekana tu mara baada ya kuchaguliwa na wabunge katika uchaguzi utaofanyika hivi karibuni.
Aidha amesema kuwa wabunge wamchague mgombea Spika Dk.Tulia kwa kura nyingi kwani maendeleo yanatakiwa kuanza kasi kwa kutegemea mhimili wa bunge.
Msama amempongeza Mwenyekiti wa Chama Rais Samia Hassan Suluhu na Kamati kuu kwa kumteua Dk.Tulia Ackson kuwa mgombea wa Uspika.
“Wanaume sasa tutulie waacheni wanawake wachape kazi kwani wakati wanaume tukiwa juu wanawake walikuwa wanaangalia tu hivyo nasi wanaume tutulie”amesema Msama.
Msama amesema kuwa watangaza nia sasa ni kuchapa kazi na kukijenga chama cha Mapinduzi na aliyeteuliwa pale atapopita afanye yale Watanzania wanayotaka.