………………………………………………….
Mkuu wa wilaya ya Ludewa Andrea Tsere ametoa maagizo kwa viongozi wote ngazi ya kata na vijiji kuhakikisha kuwa wanafuzi wote wanaotakiwa kuripoti shule wamesharipoti na waliofikia umri wa kuanza darasa la awali na lakwanza wawe wameshaanzishwa shule.
Akizungumza hayo ofisini kwake mkuu huyo wa wilaya amesema kuwa kuanzia jumatatu ya tarehe 24 mwezi huu katika maeneo yote watafanya msako wa kukagua watoto ambao wameachwa majumbani na endapo watabainika wazazi watachukuliwa hatua za kisheria.
Mkuu huyo ameongeza kuwa kuna baadhi ya maeneo viongozi wa vijiji na vitongoji wamekuwa ni sababu ya kurudisha nyuma maendeleo ya elimu kwani wamekuwa wakiungana na kuwatetea wazazi kutowapeleka watoto shule na badala yake wanabaki majumbani kwaajili ya kulea wadogo zao na kusaidia shughuli za nyumbani na mashambani.
“Haiwezekani Mwenyekiti wa kitongoji na kijiji muwe kikwazo cha maendeleo ya elimu, sasa natoa amri kwa viongozi wote ngazi ya kata na vijiji mshirikiane kwa pamoja kuhakikisha kuwa watoto wote wanaripoti mashuleni na hakuna atakayesalia nyumbani”, amesema Tsere.
Amesema msako huu haujalenga kwa wanafunzi wanaoanza shule tu, bali hata kwa wanafunzi waliokwisha kuanza wa vidato mbalimbali na madarasa mbalimbali kwani nao wakirudi likizo wamekuwa hawarudi shuleni kuendelea na masomo hivyo utawahusu pia.
“Watoto wanaporudi likizo wazazi wamekuwa wakiwatafutia kazi za ndani na vibarua mbalimbali ili wawasaidie kiuchumi sasa napenda niwajulishe kwamba umri wa mtoto wako kufanya kazi bado haujafika anapaswa kuwepo shuleni na endapo nikibaini mzazi uliyemtafutia kazi mtoto wako au kumruhusu akafanye kazi sheria itafuata mkondo wake.
Sanjali na hilo pia amewataka wazazi kupeleka chakula mashuleni kwa wakati kwaajili ya watoto wao kwani kwa kutofanya hivyo ni kuwatesa watoto wao kwa kushinda na njaa kwa muda mrefu au kutembea umbali mrefu kwenda majumbani mwao kufuata chakula.
Ameongeza kuwa awali kulikuwa hakuna uwiano mzuri wa kiwango cha kupeleka chakula mashuleni lakini kwa sasa tayari kamati ilishaundwa ya kuhakikisha kunakuwa na uwiano sawa kwa shule zote hivyo wazazi wanapaswa kuwajali watoto wao katika hilo.