Wawakilishi kutoka TANRODAS Mkoa wa Pwani wakiwa katika kikao maalum katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge akizungumza na Wawakilishi kutoka TANRODAS Mkoa wa Pwani
………………………….
SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Wakala wa Barabara nchini ( TANROADS) inatarajia kuanza kufanya kazi ya usanifu wa ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Kibaha-Chalinze-Morogoro.
Afisa Sayansi ya Jamii Mkuu kutoka TANROADS Makao Makuu, Gibson Mwaya ametoa taarifa hiyo leo Mjini Kibaha katika kikao maalum kilichofanyika katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge.
Katika kikao hicho ambacho kilimshirikisha Mkuu huyo wa Mkoa,Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Sara Msafiri pamoja na wawakilishi kutoka TANRODAS Mkoa wa Pwani, Mwaya amesema kazi hiyo itaanza mapema wiki ijayo.
Mwaya amesema kuwa, kazi ya usanifu wa ujenzi wa barabara hiyo itafanyika kwa muda wa miezi miwili na baadae ripoti ya awali itakabidhiwa kwa Mtendaji Mkuu.
Amesema,baada ya kumaliza usanifu huo ripoti hiyo itaeleza namna ambavyo kazi inapaswa kufanyika pamoja na gharama halisi za ujenzi wa barabara hiyo.
“Kazi ya usanifu wa ujenzi wa njia nne kutoka Kibaha -Chalinze -Morogoro itaanza wiki ijayo na timu ya Suveyor itapita kwenye barabara iliyopo, lakini hata hivyo wataweza kupita sehemu tofauti na barabara hiyo kulingana na michoro itakavyoonyesha,”amesema Mwaya.
Aidha,Mwaya amesema baada ya usanifu huo ndipo watapata picha kamili ya kujua nani atatakiwa kulipwa fidia na nani hawatatakiwa kulipwa na kwamba kazi ya kuhamasisha na kutoa elimu kwa wananchi itafanyika .
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayofanya na anazoendelea kuzifanya na kwamba ni vyema wananchi kwa pamoja wakaunga mkono juhudi hizo.
Kunenge,amesema barabara hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa na kwamba itakwenda kuleta uchumi imara wa Mkoa wa Pwani na huku akisema jambo hilo ni faraja kwa wananchi.
Amesema,kuwa kitendo cha Serikali kutoa fedha hasa katika kufanya Usanifu na tathimini ya mazingira kwa barabara ya Kibaha -Morogoro ni jambo la kumshukuru sana Rais wetu kwakuwa ametambua umuhimu wa barabara yetu.
Kunenge ameongeza kuwa, barabara hiyo itajengwa njia mbili kwenda na njia mbili kurudi mpaka kufika Mkoani Morogoro ikiwa sawa na kilomita 158 nakusema njia hizo zinaitwa njia za haraka (express Way).
“Kazi hiyo itakuwa na athari chanya katika nchi yetu,nchi za SADC na hata Afrika Mashariki na hata kuondoa changamoto za usafiri kwa wananchi na hii inadhihirisha namna ambavyo Rais anafanyakazi ya kimaendeleo hapa nchini,”amesema.
Amesema kuwa,Mkoa wa Pwani umepata bahati kubwa ya kuwa na miradi mingi ya ujenzi kwani ukiachilia mbali barabara ya Kibaha -Morogoro lakini bado kuna miradi mingine mikubwa ya ujenzi wa daraja la Wami na barabara ya kwenda Bandari kavu ya Kwala.
Kunenge,amesema barabara ya Vigwaza- Kwala kuelekea katika Bandari kavu Rais ametoa kiasi cha Sh.bilioni 31 na ujenzi unaendelea lakini daraja la Wami linajengwa kwa gharama ya bilioni 72 na ujenzi upo hatua za mwisho.
“Kwakweli lazima tumpongeze Rais kwa kazi hizi kubwa na jinsi ambavyo anautazama Mkoa wa Pwani kwakuwa Pwani kuna viwanda vingi na barabara hiyo itakuwa msaada mkubwa kwa wananchi hasa kupunguza foleni,”ameongeza.
“Uwezo wa barabara hii kuhimili magari ni mdogo, lakini niseme Serikali imeliona hilo na tayari imetenga fedha kwa ajili ya usanifu na hii itaondoa changamoto kwa watumiaji wa barabara hii,”amesema.
Kunenge ametoa wito kwa wakazi wa Mkoa wa Pwani hususani Kibaha watoe ushirikiano kwa timu ya wataalamu itakayopita kufanya usanifu ili kazi hiyo ikamilike kwa wakati huku akiomba wananchi waendelee kumuombea Rais Samia ili aendelee kuwatumikia Watanzania.