Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke, Bw. Christopher Myava,akizungumza na wanahabari (hawapo pichani)
…………………….
NA NOEL RUKANUGA,DAR ES SALAAM
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke wameanza uchunguzi wa malalamiko 96 yanayohusu rushwa, uku majalada 7 uchunguzi wake ukiwa umekamilika, 11 yamefungwa kwa kukosa ushahidi na 78 uchunguzi wake unaendelea.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mkoa wa Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya utekelezaji katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia mwezi Oktoba hadi Disemba 2021, Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke, Bw. Christopher Myava, amesema kuwa waliolalamikiwa ni taaasisi mbalimbali za umma pamoja na watu binafsi.
Bw. Myava amesema kuwa kuna jumla ya mashauri 22 yanaendelea kusikilizwa katika Mahakama ya Mkoa wa Temeke.
Hata hivyo amebainisha kuwa pamoja na kuendelea na majukumu yao ya kila siku kuanzia mwezi huu January hadi machi wanaongeza kasi ya ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo ili kuziba mianya hasa katika ujenzi wa miradi ya maendeleo.
‘ katika kipindi cha Januari –Machi mwaka huu tutahakikisha tunaongeza kasi ya ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo ili kuziba mianya hasa katika ujenzi wa miradi ya maendeleo ambayo serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi’amesema Myava
Bw. Myava amesema kuwa bado Kuna shida kwenye thamani ya fedha kwa miradi inayotekelezwa kutokana mingi haifanani na fedha zinazotolewa.
Amesema kuwa TAKUKURU Mkoa wa Temeke wanaendelea kutoa elimiu kupitia Makundi mbalimbali yenye kuhamasisha wananchi ili kuongeza uelewa katika mapambano dhidi ya rushwa.