Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko,akizungumza na wachimbaji wadogo katika Mgodi wa Mahagi uliopo Wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita.
Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko,akiendelea na kukagua Mgodi wa Mahagi uliopo Wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita.
Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuzungumza na wachimbaji wadogo katika Mgodi wa Mahagi uliopo Wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita.
WACHIMBAJI wadogo wa madini nchini wametakiwa kuachana na migogoro inayosababisha kusimama kwa shughuli zao na wajikite katika shughuli za uchimbaji zenye tija kwa Taifa.
Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko ametoa wito huo alipotembelea na kuzungumza na wachimbaji wadogo katika Mgodi wa Mahagi uliopo Wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita.
Akizungumzia eneo la mgogoro katika Mgodi wa Dhahabu wa Mahagi, Dkt. Biteko amesema, mgogoro wa umiliki wa mashamba kati ya familia ya ndugu Gervas Bambo na Saanane Jagi unachangia kuathiri shughuli za uchimbaji.
“Ndugu zangu Watanzania, dhahabu haichimbwi kwa migogoro, dhahabu inachimbwa kwa kufanya kazi,” amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza kuwa, ili Sekta ya Madini iweze kukua,migogoro kwa wachimbaji inapaswa kuondolewa.
Pia, amewataka wachimbaji wapendane na kupunguza chuki ili wafanye shughuli zao kwa faida.
Dkt. Biteko amewataka kuacha kuzushia viongozi kwa kuwapa tuhuma mbalimbali. Amesema, maneno yanayozungumzwa kwa wasimamizi hao yanazorotesha ustawi wa Sekta ya Madini kwa ujumla.
Aidha, amewataka viongozi wa Serikali na wa kisiasa kuacha kuchochea migogoro. Amesema, mgogoro huo ulianza kwa viongozi wa Kata ya Izunya na Karuma baada ya dhahabu kupatikana katika eneo hilo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale, Jamhuri William amempongeza Dkt. Biteko kwa kuanzisha Mkoa wa Kimadini wa Mbogwe. Amesema, uwepo wa mkoa huo utasaidia usimamizi wa shughuli za madini kwa kuongeza mapato katika Halmashauri ya Nyang’hwale na pato la Taifa.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Nyang’hwale,Hussein Amare amesema, ziara ya Dkt.Biteko katika jimbo hilo imesaidia kupunguza migogoro ya wachimbaji hususan maeneo yenye mlipuko wa madini ya dhahabu.
Ziara ya kuzungumza na kutembelea maeneo ya wachimbaji wadogo ya Dkt. Biteko ilihudhuriwa na viongozi wa Serikali na chama, wadau mbalimbali wa Sekta ya Madini ambapo wachimbaji waliuliza maswali na kupewa ufafanuzi kuhusu masuala mbalimbali ya sekta.