Waombolezaji wakiuswalia mwili wa Marehemu Steven Rehema Kazidi kabla ya mazishi yaliyofanyika Chalinze mkoani Pwani.
Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mzee Jakaya Kikwete akizungumza na Katibu Mwenezi wa CCM Taifa Ndugu Shaka Hamdu Shaka walipokutana katika msiba wa Kada wa CCM Marehemu Mzee Steven Kazidi ambaye amezikwa Leo Chalinze mkoani Pwani.
Rais Mstaafu Mzee Jakaya Mrisho Kikwete akiweka udongo kwenye kaburi la Marehemu Steven Kazidi wakati wa mazishi yake yaliyofanyika Chalinze Leo.
Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete akitoa Salam zake kwa waombolezaji wakati aliposhiriki shughuli za mazishi hayo.
Katibu Mwenezi wa CCM taifa Ndugu Shaka Hamdu Shaka akitoa Salam za chama wakati wa mazishi ya Kada wa CCM Marehemu Steven Kazidi ambaye amezikwa Leo Chalinze mkoani Pwani.
…………………………………
Viongozi, Wanachama, watumishi wa CCM, wapenzi, wakereketwa wa CCM na wananchi mbali mbali Jumatatu 03 Januari 2022, wamehudhuria mazishi ya aliyekuwa mwanachama, mtumishi, kiongozi na kada mahiri wa CCM Mzee Steven Rehema Kazidi kijijini kwao Vigwaza, Chalinze mkoani Pwani, ambae alifariki Januari 1 2022 katika hospitali ya Mloganzila alipokuwa akipatiwa matibabu.
Pamoja na viongozi wengine mazishi hayo pia yamehudhuriwa na *Rais Mstaafu wa Awamu ya nne Ndugu Jakaya Mrisho Kikwete.*
Akitoa Salaam za rambirambi za Chama Cha Mapinduzi kwa niaba ya Katibu Mkuu wa CCM, Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Shaka H. Shaka alisema
*”Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ndugu Samia Suluhu Hassan amemuelezea Marehemu Kazidi kuwa wakati wa uhai wake alikuwa mwanachama, Kada, kiongozi na mtumishi wa CCM mahiri, mbunifu, aliyekuwa na moyo wa kujitoa na kujitolea Muda wote, vipawa na nguvu zake kukijenga na kuitumikia CCM na wananchi kwa uamininifu na utiifu mkubwa”*
*”Mzee Kazidi alikuwa na sifa ya unyenyekevu na ulezi kwa vijana katika uongozi. Hivyo CCM, tumempoteza mwanachama, kada mahiri, mlezi na mwalimu wa siasa na uongozi kwa vijana”* Alisisitiza Shaka.
Wakati wa uhai wake Mzee Stephen Rehema Kazidi alitumikia nafasi mbali mbali kwa nyakati tofauti ikiwemo Mwenyekiti wa kijiji cha Vigwaza, Diwani wa Kata ya Vigwaza, Mwenyekiti wa Halimashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Katibu wa Siasa na Uenezi Wilaya ya Bagamoyo, Katibu wa CCM Wilaya, Ukatibu wa CCM Mkoa na Katibu Msaidizi Mkuu Idara ya Oganaizesheni CCM Taifa.
Viongozi wengine mbalimbali wa Chama na serikali walishiriki ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Pwani, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo na Kilosa watumishi wa CCM toka Makao Makuu Ofisi Ndogo Lumumba, Mkoa wa Pwani na Morogoro.
Sote ni wa MwenyeziMungu na kwake tutarejea .