Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza katika Kijiji Cha Kagongo Kigoma wakati allpokagua nyumba ya mganga iliyojengwa na TASAF.
Baadhi ya wananchi wa Kijiji Cha Kagongo mkoani Kigoma wakishuhudia nyumba ya mganga iliyojengwa kijijini Hao na TASAF.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema TASAF imejenga nyumba ya Mganga katika Kijiji cha Kagongo, Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma kwa lengo la kuwawezesha wananchi kupata huduma kwa wakati katika Zahanati ya kijiji hicho.
Akizungumza na wananchi na walengwa wa TASAF katika Kijiji cha Kagongo, Mhe. Mchengerwa amesema, ujenzi wa nyumba hiyo umewaondolea adha wananchi wa kijijiji hicho ya kuchelewa kupata huduma kwani Mganga aliyekuwa akiwahudumia alilazimika kusafiri takribani kilomita kumi kila siku ili kutoa huduma kwa wananchi wa kijiji hicho.
“Tumefanikisha ujenzi wa nyumba hii, Mganga anaishi hapa na huduma zinatolewa kwa wakati, hii ndio dhamira ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwasogezea huduma wananchi,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.
Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa, Serikali kupitia TASAF itaendelea kuboresha huduma za kijamii ili wananchi waweze kunufaika na huduma zinazotolewa na Serikali yao kama ambavyo Rais wa Awamu ya Sita, Mhe. Samia Suluhu Hassan amedhamiria.
Katika kuhakikisha dhamira hiyo inatekelezwa, Mhe. Mchengerwa amesema, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ametoa fedha za kutosha kuwezesha upatikanaji wa huduma za kijamii katika maeneo yote yenye uhitaji.
“Nataka niwatoe hofu Watanzania wenzangu waliokuwa wanafikiri mradi huu wa TASAF hautaendelea, napenda niwaambie kuwa, Rais wetu ametupatia kiasi cha shilingi trilioni 2.03 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya TASAF, hii ina maana kuwa, tutazifikia kaya zote maskini nchini ambazo hazikufikiwa na mpango katika awamu zilizopita,” Mhe. Mchengerwa ameongeza.
Mhe. Mchengerwa anaendelea na ziara ya kikazi mkoani Kigoma ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.