*******************
Na. Projestus Binamungu
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa ameshiriki uzinduzi wa Mintape iliyopewa jina la Kitimoto yenye nyimbo tisa za msanii wa kizazi kipya kutoka kundi la wanamuziki la Weusi George Mdeme ‘G Nako,’ akiwataka wasanii kuendelea kushirikiana licha ya ushindani unaoitawala kazi yao.
Katika tukio hilo lililoenda sambamba na uzinduzi wa ofisi mpya za kituo cha redio cha A.FM cha Jijini Dodoma, Waziri Bashungwa amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kwa kundi hilo muhimu katika jamii akisema ni kutengeneza jamii mpya yenye ushirikiano katika kukuza mziki.
Katika hatua nyingine Waziri Bashungwa ameupongeza uongozi wa A. Fm pamoja na kundi la Weusi kwa kufanya uzinduzi wa tukio hilo kubwa Jijini Dodoma akisisitiza kuwa Dodoma ni makao makuu ya nchi hivyo lazima Serikali na wadau wengine washirikiane katika kuikuza kiburudani ili kuwaburudisha watanzania wote.
Kwa upande wake G Nako, amesihukuru Serikali kupitia kwa Waziri Bashungwa, akisema ushiriki wa viongozi wa ngazi za juu katika matukio yanayo wahusu wasanii, ni ushahidi jarabati kuwa sasa wanasikilizwa na kero zao zinatatuliwa.