Waziri wa Fedha na Mipango wa Tanzania Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (katikati) akimtambulisha Waziri wa Fedha wa Zanzibar Mhe. Jamal Kassim Ali (kushoto kwa Waziri wa Fedha wa Misri Dkt. Mohamed Maait, mjini Cairo nchini Misri walipokutana kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili katika sekta ya fedha na uchumi.
Waziri wa Fedha wa Misri Dkt. Mohamed Maait, akimkabidhi Waziri wa Fedha na Mipango wa Tanzania Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba zawadi ya kitabu chenye maelezo ya Makumbusho ya Taifa ya nchi hiyo, Mjini Cairo, Misri.
Waziri wa Fedha wa Misri Dkt. Mohamed Maait, akimkabidhi Waziri wa Nchi-Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Jamal Kassim Ali, zawadi ya kitabu chenye maelezo ya Makumbusho ya Taifa ya nchi hiyo, Mjini Cairo, Misri.
Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (katikati) ukiwa katika majadiliano ya namna ya kuimarisha uhusiano na Jamhuri ya Kiarabu ya Misri na Ujumbe wa Wizara ya Fedha ya Misri ukiongozwa na Waziri wa Fedha wan chi hiyo Dkt. Mohamed Maait (kulia).
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akisisitiza jambo wakati wa majadiliano na Mwenyeji wake, Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri Dkt. Mohamed Maait (hayupo pichani), walipokutana Mjini Cairo kujadili fursa zilizopo katika nchi hizo mbili katika masuala ya kodi na uchumi. (picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)
……………………………………………………………
Na Benny Mwaipaja, Cairo
TANZANIA na Misri zimekubaliana kuondoa changamoto ya utozaji wa kodi mara mbili kwenye bidhaa zinazoingia au kutoka katika nchi hizo mbili ili kusisimua biashara na kukuza mauzo nje ya nchi yatakayoongeza upatikanaji wa fedha za kigeni.
Waziri wa Fedha na Mipango wa Tanzania Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba amesema hayo baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha wa Misri Dkt. Mohamed Maait, mjini Cairo nchini Misri.
Mawaziri hao wa Fedha wa Tanzania na Misri wameafikiana kushirikiana katika nyanja mbalimbali za kukuza uchumi wa nchi hizo mbili ikiwemo kutangaza fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini Tanzania.
“Tumekubaliana kuendeleza ushirikiano katika eneo la kujengeana uwezo katika masuala ya kikodi lakini pia tutasaini makubaliano ya kuondoa utozaji wa kodi mara mbili kwenye bidhaa zinazotoka kwenye nchi zetu” alisema Dkt. Nchemba
Alisema kuwa Tanzania na Misri zina uhusiano wa kimkakati na hivi sasa mkandarasi anayejenga mradi mkubwa wa uzalishaji umeme wa Bwawa la Nyerere anatoka Misri na kwamba katika eneo hilo wamekubaliana namna ya kufanikisha mradi huo ikiwemo kutafuta fedha za kuukamilisha.
Dkt. Nchemba alisema kuwa wamekubaliana pia kutafuta wawekezaji watakao leta teknolojia na mitaji nchini Tanzania kwa kuwekeza kwenye maeneo yatakayotumika kuzalisha ikiwemo sekta ya kilimo.
“Hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan aliwapokea wawekezaji kutoka nchini Misri, tunaweza kutumia fursa za uhaba wa ardhi kwenye nchi yao kuwavuta kuja kuwekeza kwenye shughuli za kilimo kupitia vyanzo vya fedha za kigeni kutoka kwenye kampuni zao” Aliongeza Dkt. Nchemba.
Aliongeza kuwa wamejadili na kuangalia namna ya kutumia nishati ya gesi inayozalishwa nchini Tanzania kuzalisha umeme kutokana na uzoefu wa nchi hiyo katika eneo hilo la matumizi ya gesi hatua iliyoifanya kuzalisha nishati ya umeme kwa wingi na ziada kuuza nchi za nje.
“Wana maslahi katika jambo hilo kwa sababu litapunguza pia uharibifu wa mazingira na kusaidia maji mengi kwenda Ziwa Victoria, maji ambayo yanatumiwa na nchi yao kwa hiyo kuna mambo mengi yanayotuunganisha” alisisitiza Dk. Nchemba
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango-Zanzibar Bw. Jamal Kassim Ali alisema kuwa suala la kuhimiza uwekezaji kutoka nchini Misri lilipewa kipaumbele na kutaja fursa ambazo nchi itanufaika kutokana na uwekezaji huo.
“Misri ni moja ya nchi zilizoendelea sana katika masuala ya ujenzi wa miundombinu kwahiyo tumeona tuna fursa kubwa ya kufanyakazi na kampuni kubwa za Misri kwa kujenga na kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo” alisema Bw. Ali.
Alisema kuwa walimweleza Waziri wa Fedha wa Misri Dkt. Mohamed Maait kuhusu fursa mbalimbali za uweezaji zilizoko Zanzibar na Tanzania kwa ujumla na kwamba wanatarajia masuala ya uwekezaji na biashara yatafunguka zaidi kwa manufaa ya pande zote mbili.
Waziri wa Fedha na Mipango wa Tanzania Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba akisalimiana na Waziri wa Fedha wa Misri Dkt. Mohamed Maait, mjini Cairo nchini Misri walipokutana kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili katika sekta ya fedha na uchumi.