
MAGWIJI wa Muziki wa Dansi nchini,Ali Choki, Prince Muumini Mwinyijuma na Abubakar Manjegeka, watapanda jukwaa moja Villa Park Resort jijini Mwanza kukumbushia enzi zao kwa vijana wa sasa baada ya watani wa jadi Simba na Yanga kuonyeshana kazi.
Wanamuziki hao watasindikizwa na wasanii wa kike Catherine Lukamay na Lucy Lukumay ambao wataonyeshana kazi kuimba tungo zilizoimbwa na Luiza Mbutu,Hadija Mnonga au Kimobitel, Jesca Charles na marehemu Amina Ngaluma.
Onyesho hilo litafanyika Jumamosi usiku, Villa Park Resort likiwa mahususi kwa ajili ya kusindikiza sherehe za miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika .
Meneja wa Villa Park Resort, Benard James alisema kuwa wadau wa muziki wa dansi watajipoza kwa burudani itakayoshushwa na wanamuziki hao watakaopanda jukwaa moja kutoa burudani kwa wapenzi na wadau wa muziki huo jijini Mwanza.
Alisema onesho hilo litalowahusisha magwiji hao watatu wakisindikizwa na wanumuzi wawili wa kike mbali na kutoa burudani ni mahususi kwa ajili ya sherehe za Uhuru na lenye lengo la kuwaonyesha vijana utunzi wa wanamuziki wa zamani ili nao waige .
” Wasanii wa zamani wajituma na walijitahidi kufanya muziki ambao umeishi kwa muda mrefu bila kuchuja,tunataka vijana wa kizazi cha sasa waige kupitia kwa magwiji hao,”alisema James.
Aliongeza katika kunogesha onyesho hilo wanamuziki chipukizi wa kike Lucy Lukamay na Catherine Lukamay, watakuwa na kazi ya kukonga nyoyo za wadau wakiwakumbusha enzi za Luiza Mbutu, Hadija Mnonga ‘Kimobitel’,Jesca Charles na marehemu Amina Ngaluma.
Wasanii hao wataimba nyimbo zilizowapa umaarufu wanamuziki hao waliowahi kutamba nchini wakiwa na bendi mbalimbali.
Wasanii hao wa kike watapamba jukwaani sambamba Mzee wa Kijiko ama Farasi, Ali Choki ambaye ataimba nyimbo zake zilizompa umaarufu tangu akiwa nchini Kenya kisha nyumbani Tanzania akiwa na bendi mbalimbali.
Pia mwanmuziki kipofu, Abubakar Manjegeka wa bendi ya Villa Park Musica ataonyedha kipaji na uwezo wake wa kuimba nyimbo za marehemu Banza Stone huku Prince Mwinyijuma akitarajiwa kukonga nyoyo za wadau wa muziki huo kwa kupiga vibao vyake vya zamani vilivyompa umaarufu