Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Jomaary Satura.
Muonekano wa moja ya barabara za Manizspaa ya Shinyanga.
………………………………..
Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
WAKAZI wa Manispaa ya Shinyanga wamempongeza mkurugenzi wa manispaa hiyo Jomaary Satura kwa kuuweka mji katika mazingira safi ambapo wameahidi kuunga mkono jitihada hizo huku wakimuomba kuanza kutekeleza matumizi ya sheria ya usafi wa mazingira ili kudhibiti watu wanaochangia uchafuzi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wamesema mkurugenzi huyo amekuja na kasi mpya na msukumo wa maendeleo ambapo eneo la usafi wa mazingira limekuwa na usimamizi mzuri hali inayoufanya mji wa Shinyanga kuonekana katika mandhari nzuri.
Wamemuomba mkurugenzi huyo kuanza kutumia sheria ya usimamizi wa usafi wa mazingira ili kuwadhibiti wale wote watakaobainika kuhusika na uchafuzi wa mazingira ikiwa ni pamoja na kuweka vyombo maalum vya kuhifadhi taka katika maeneo mbalimbali.
Aidha wananchi hao wamemuomba bwana afya pamoja na maafisa afya kujenga utaratibu wa kuwatembelea mara kwa mara kwa lengo la kujilidhisha hali ya usafi wa mazingira.
Hivi karibuni wakati akizungumza na vyombo vya habari mkuu wa Idara ya Usafi na Mazingira Manispaa ya Shinyanga Kuchibanda Snatus amesema sheria ya usimamizi usafi wa mazingira itaanza kutumika hivi karibuni .
“Sheria ipo inasema ikitokea mtu akashindwa au amekaidi anatakiwa atozwe faini isiyozidi sh,50,000 au afikishwe mahakamani” amesema.