Mratibu wa Mradi wa maji wa Tabora, Igunga Nzega, Mhandisi Edwin Mlumba pamoja na Mkuu wa Idara ya Mipango, Sera na Utafiti Wizara ya Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Abdulrabi Juma wakijadiliana jambo wakati wa ziara ya kutembelea mradi wa maji wa Tabora, Igunga, Nzega
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Nzega Athmani kilundumya akitoa maelezo kuhusiana na mradi..
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tabora Benard Biswalo akitoa maelezo ya mradi huo katika eneo la tenki la mradi lililoko eneo la Kaze Hill mjini Tabora
Tenki la mradi eneo la Nzega
Msimamizi wa Uhawilishaji na Uimarishaji wa Mfumo wa Usambazaji Maji Zanzibar, Abdulmalik Hassan Ally akichungulia moja ya eneo la miundombinu ya mradi
Wataalamu wakikagua tenki la mradi mjini Igunga
…………………………………………………………………
Wataalamu wa sekta ya maji Tanzania Bara na Zanzibar wamepongeza makubaliano ya ushirikiano wa pamoja katika kutatua changamoto zinazoikumba sekta ya maji hapa nchini.
Pongezi hizo zimetolewa na wataalamu wa sekta ya maji wa pande mbili za Muungano mara baada ya wataalamu kutoka Zanzibar kutembelea mradi wa maji wa Tabora, Igunga, Nzega kwa lengo la kujifunza namna mradi huo ulivyotekelezwa kwa haraka na kwa ufanisi mkubwa.
Akizungumza kuhusu utatuzi wa changamoto Msimamizi wa Uhawilishaji na Uimarishaji wa Mfumo wa Usambazaji Maji Zanzibar, Abdulmalik Hassan Ally amesema ushirikiano huo ni hatua moja muhimu kufikia suluhu za pamoja katika kutatua changamoto zinazoikumba sekta. Amesema changamoto nyingi za utekelezaji wa miradi ya maji kwa pande mbili za Muungano zinafanana hivyo ushirikiano wa pamoja utawezesha muafaka wa haraka katika kufikisha huduma ya maji kwa wananchi.
Amewapongeza Wizara ya Maji kwa kufanikisha utekelezaji wa miradi mikubwa ukiwemo huo wa Tabora, Igunga hadi Nzega huku akijivunia kupata maarifa mapya ambayo watayatumia huko Zanzibar ili kufanikisha shughuli zao.
Kwa upande wake Mratibu wa utekelezaji wa mradi wa maji wa Tabora, Igunga Nzega Mhandisi Edward Mlumba amesema mradi huo wenye thamani zaidi ya Bilioni 600 ulitekelezwa na kukamilika kwa wakati kutokana na usimamzi mzuri wa timu nzima ya utekelezaji na usimamizi kuanzia ngazi ya Wizara, Mkandarasi na jamii ya maeneo ulikotekelezwa mradi.
Amesema kampuni tatu zilizotekeleza mradi huo ndizo ambazo zinatekeleza mradi huko Zanzibar hivyo ujio wa Wataalamu hao kutoka Zanzibar utasaidia kufahamu ni namna gani wao waliweza kufanikisha utekelezaji wake kwa wakati.
Ziara ya Wataalamu wa Sekta ya maji kutoka Zanzibar inakuja kufuatia makubaliano ya pamoja kwa wizara mbili zinazohusika na utoaji wa huduma ya maji kwa kila upande wa muungano kukubalina kushirikishana utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazoikumba sekta hiyo.