Mchezaji chipukizi Isack Daudi kutoka Klabu ya Gofu ya Lugalo akikabidhiwa kombe na Naibu Katibu Mkuu Dkt. Ally Possi baada ya kuibuka mshindi wa jumla mashindano ya Golfu ya NBC Tanzania Open 2021 jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo. Dkt, Ally Possi usiku wa Disemba 5, 2021 akitoa hotuba ya kufunga rasmi mashindano ya Golfu ya NBC Tanzania Open 2021 jijini Dar es Salaam
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo. Dkt, Ally Possi usiku wa Disemba 5,2021 akikabidhiwa kanuni za mchezo wa Gofu na Mwenyekiti wa Klabu ya Jeshi ya Lugalo Brigadia Generali Mstaafu, Michael Luwongo baada ya kutangaza nia ya kujifunza mchezo huo.
*************
Na. John Mapepele
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo. Dkt, Ally Possi usiku wa Disemba 5, 2021 amefunga rasmi mashindano ya Golfu ya NBC Tanzania Open 2021 jijini Dar es Salaam na kukabidhiwa kanuni za mchezo huo na Mwenyekiti wa Klabu ya Jeshi ya Lugalo Brigadia Generali Mstaafu, Michael Luwongo baada ya kutangaza nia ya kujifunza mchezo huo.
Katika mashindano hayo mchezaji chipukizi Isack Daudi kutoka Klabu ya Gofu ya Lugalo ameibuka kuwa mshindi wa jumla mashindano ya mwaka 2021.
Akifunga mashindano hayo, Dkt. Possi amepongeza vilabu kwa kuanza kuwekeza na kuibua vipaji kwa watoto ambao wameshiriki mashindano ya mwaka huu kwa mara ya kwanza na kufanya vizuri.
Akimkaribisha kufunga mashindano hayo, Mwenyekiti wa Chama cha Gofu Tanzania (TGU), Chriss Martin ameiomba Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kudhamini wa Timu ya Taifa ya mchezo wa Gofu ili iweze kufanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa na pia ameomba kiwanja kwa ajili ya mchezo huo.
Akijibu maombi hayo, Dkt. Possi amefafanua kuwa Serikali ina mikakati kabambe ya kuendeleza michezo ikiwa ni pamoja na kutoa udhamini kwa timu za taifa za michezo zinazofanya vizuri kupitia Mfuko wa Michezo ulioanzishwa hivi karibuni endapo zitakuwa zimekidhi vigezo vilivyowekwa.
Ameongeza kuwa Serikali pia itazingatia kigezo cha utawala bora kwenye vyama na mashirikisho ya michezo katika kudhamini michezo. Ametoa wito kwa vyama kuwa na utawala bora ili kufika katika ngazi ya kimataifa.
Akizungumzia kuhusu kiwanja amesema Serikali ipo tayari kuwatafutia kiwanja kwa ajili ya Gofu ambapo amesisitiza kuwasilisha maombi rasmi yafanyiwe kazi ili wapatiwe kiwanja hicho.
Akitoa Salamu za Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Innocent Bashungwa amesema amemuagiza TGU kukutana mara moja na Mhe. Waziri Bashungwa ili kujadiliana namna ya kuuendeleza mchezo huo pendwa ambao umeonyesha kukuwa kwa haraka hapa nchini.
Katibu wa mashindano hayo, Mhandisi Enock Magile amesema TGU katika kuendeleza mchezo huo kimeandaa michezo maalum ya Gofu kwa akina mama itakayofanyika mwakani.
Aidha amesema Aprili 2022, Tanzania itakuwa mwenyeji wa shindano la kimataifa la mchezo wa Gofu la Europen Tour Challenge litakalowaleta wachezaji wa kimataifa 159 kutoka mataifa mbalimbali duniani watakaoambatana na wageni 559 ambapo amefafanua kuwa litasaidia kukuza utalii.