Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akizungumza baada ya kumalzika kwa mkutano wa nane wa Mawaziri wa Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC)
……………………………………………………..
Na Mwandishi wetu, Dakar
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) amesema mkutano wa Nane wa Mawaziri wa Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) kimefanyika kwa mafanikio makubwa.
Balozi Mulamula ametoa kauli hiyo jijini Dakr nchini Senegal baada ya kumalizika kwa kikao hicho kilichofanyika Novemba 29 na 30 2021 nchini humo.
Amesema kikao hicho kimekuwa cha mafanikio kwani kimepitisha maazimio makubwa na mpango kazi ambao umejikita katika kutekeleza maeneo ya kimkakati ambayo yakisimamiwa kikamilifu yatazinufaisha nchi za Afrika .
Balozi Mulamula amesema kauli ya China ya kuzihakikishia nchi za Afrika kuwa itasaidia kuanzisha viwanda vya kuzalisha chanjo za COVID 19 pamoja na dawa nyingine ni ya kujivunia na ya kupongezwa.
“Tanzania imefurahishwa na ahadi hiyo kwani jambo hilo litazifanya nchi za Afrika kuwa na uwezo wa kuzalisha chanjo na dawa nyingine kwa ajili ya kuwalinda watu wake na kuacha kutegemea msaada., kauli ya Rais Jinping ni ya kujivunia na ya lupongezwa,”amesema Balozi Mulamula.
Amesema kikao kimekuwa na mafanikio zaidi kwani mbali na kuangalia maeneo ya siku zote ya kuendeleza miundombinu na viwanda, kwa mara ya kwanza umeangalia jinsi ya kusaidia na kuendeleza wafanyabiashara wadogo na wa kati.
Amesema uamuzi wa China kwa kutoa kipaumbele katika eneo la kujenga viwanda vya kuzalisha dawa na chanjo na kuwawezesha wafanyabiashara wadogo na wa kati ni wa kupongezwa mno kwani mambo hayo ndiyo ambayo Tanzania ilitilia mkazo katika taarifa yake na kuongeza kuwa wamefarijika kwamba Rais Jinping ameahidi kusaidia katika eneo hilo.
“Jambo hili ni zuri na kubwa sana, ni miongoni mwa maeneo ambayo Tanzania iliyasemea, eneo hilo ndiko watu wengi walikopata ajira hasa akina mama na vijana tunaishukuru na kuipongeza China kwa kutoa kipaumbeele katika eneo hilo”, alisema Mhe. Waziri.
Amesema kikao hicho pia kimeangalia maeneo ya kujengea uwezo wananchi wa Afrika katika eneo la ufadhili wa masomo ambalo kwa wakati huu limekwama kutokana na mlipuko wa virusi vya Covid 19 lakini wameahidi kuendelea nalo pale hali itakapotengemaa.
Ameongeza kuwa kikao pia kimeangalia suala la kuendeleza kilimo ili kuwa na kilimo cha kisasa na kuendeleza miundombinu ya kidijitali hasa nyakati hizi ambazo ni lazima kujiunganisha kidigitali ili kujikwamua kiuchumi.
Amesema China imesisitiza na kuweka mkazo katika eneo la kundeleza kilimo ili kuziwezesha nchi za Afrika kujikwamua na umasikini na wameahidi kutoa fedha na kuleta wataalamu kwa ajili ya kuendeleza kilimo.
Mkutano huo wa siku mbili ulijumuisha viongozi na wawakilishi kutoka Bara la Afrika na China uliangalia jinsi China ilivyotekeleza hatua za ushirikiano kwa kipindi cha miaka mitatu cha 2018-2021 kwenye maeneo ya miradi ya kimkakati na ukuzaji wa wigo wa biashara kati ya China na mataifa ya Afrika.