Programu Meneja wa Shirika la CAMFED Tanzania, Anna Sawaki (kulia) akizungumza katika mkutano huo uliofanyika Ukumbi wa Msimbazi Center jijini Dar es Salaam. |
Mwalimu Mshauri wa Wanafunzi Shule ya Sekondari Viwege Ilala, Bi. Ruth Saibull akizungumza na wanahabari mara baada ya mkutano huo kuchangia maoni yake kufuatia uamuzi wa Serikali. |
Learnerguide wa CAMA, Bi. Mzizi Rashidi akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mkutano huo kuelezea namna watakavyoshiriki kusaidia utekelezaji wa agizo la Serikali. |
Mkurugenzi wa CAMFED Tanzania, Bi. Lydia Wilbard (wa pili kulia) akifurahi pamoja na wasichana waliosomeshwa kwa msaada na Shirika la CAMFED, ambao kwa sasa wamepata shahada mbalimbali. |
Na Joachim Mushi, Dar
SHIRIKA lisilo la kiserikali la CAMFED Tanzania limeipongeza Serikali na kuunga mkono uamuzi wa kuwarejesha shuleni wanafunzi wote waliokatiza masomo kutokana na sababu mbalimbali wakiwemo wanafunzi waliopata ujauzito wakiwa shuleni.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa CAMFED Tanzania, Bi. Lydia Wilbard kwenye Mkutano Mkuu wa mwaka wa watoto wasichana waliosomeshwa na Shirika la CAMFED, alisema uamuzi wa Serikali ni mafanikio makubwa katika sekta ya elimu kwani umefungua fursa kwa kundi hilo la jamii kurejea shuleni na kupambania ndoto zao.
Alisema CAMFED inaamini kurejeshwa kwa wanafunzi hao shuleni kwenye mfumo rasmi ni mafanikio makubwa, kwani ni jambo ambalo lilikuwa kikwazo kikubwa hasa kwa wanafunzi wa kike ambao ndio waliokuwa waathiriwa wakubwa kwa sababuza kupata ujauzito.
“Sisi kwetu ni kitu kikubwa sana, unajua tumefanya michakato mingi, tumeshiriki katika mijadala mbalimbali kupambania hii fursa kupitia kwenye mtandao wetu wa elimu TEN/MET na pia kama CAMFED kwa kushirikiana na jamii tumejaribu kuonesha ni lini mtoto anapopata ujauzito na kuacha masomo jamii itaamini ni sababu za kutowajibika vema kwa jamii husika (watu wazima),” alieleza Bi. Lydia Wilbard katika mkutano huo.
Alisema CAMFED inaamini hatua ya Serikali inaonesha wazi kuwa changamoto zilizokatisha masomo ya wanafunzi hao zimechangiwa na jamii inayowazunguka kwa kushindwa kuwajibika ipasavyo.
Aidha aliongeza kuwa uamuzi huo wa Serikali kurejesha kundi hilo la wanafunzi kwenye mfumo rasmi kumeongeza wigo kwa wanafunzi waliokubwa na vikwazo kwenye masomo kabla ya kukatizwa masomo hivyo wanapata fursa ya kuamua wenyewe kulingana na mazingira na pia ndoto zake kwamba arejee katika mfumo upi kati ya rasmi na usio rasmi kumalizia masomo yao.
Hata hivyo, amebainisha kuwa suala la Serikali kutoa tamko hilo ni moja, lakini utekelezaji wake ni eneo lingine ambapo wao kama wadau wanashiriki kuangalia ni nini cha kufanya ili kuhakikisha utekelezaji unafanikiwa na hatimaye wanafunzi hao wanarejea masomoni na kukamilisha ndoto zao kielimu.
“Mimi nafikiri sasa tujikite kwenye utekelezaji…Serikali, wanajamii, sisi wakereketwa wa elimu, wasichana wenyewe, vijana tuanze kujipanga ni namna gani tunatekeleza suala hili na lifanikiwe, tusikae madarasani kusubiri wanafunzi hao warejee wenyewe kwani hawata kuja,” alisema Bi. Wilbard.
Wito wetu kama CAMFED kila mmoja wetu alichukulie suala hili kwa mtazamo chanya na kisha kushiriki katika utekelezaji wake, kila mmoja wetu afanye ni jukumu lake hivyo kuchukua hatua sehemu alipo.
“Mfano viongozi wa dini wapaze sauti kwenye nyumba za ibada kushawishi jamii kuunga mkono suala hilo kwa vitendo, wanasiasa nao walisemee suala hili kupitia majukwaa yao, viongozi wa shule nao walitangaze vizuri suala hili na pia kuangalia namna nzuri ya kudhibiti vitendo vya unyanyapaa kwa wanafunzi watakao rejea shuleni.” Alisisitiza Mkurugenzi huyo wa CAMFED Tanzania.
Kwa mujibu wa tamko la Waraka namba 2 wa Mwaka 2021 Serikali hivi karibuni ililiridhia kuwarejesha shuleni wanafunzi wote waliokatiza masomo kutokana na sababu mbalimbali kama vile utoro, utovu wa nidhamu na kupata ujauzito.