………………………………………………………
Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
MKUU wa mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge amejivunia ,mkoa huo kufikia Jumla ya viwanda 1,438 ambapo kati ya hivyo 82 ni viwanda vikubwa hali inayosababisha mkoa huo kuendelea kujinasibu kwa wingi wa viwanda vipya nchini.
Aidha ameendelea kukemea uvamizi wa ardhi zenye hati miliki zinazomilikiwa kihalali huku akitoa salamu kwa wavamizi wanaoendelea kujenga katika maeneo hayo kuacha Mara moja kabla Sheria haijachukua mkondo wake.
Akizungumza masuala mbalimbali ya maendeleo ya Mkoa ,katika kikao cha ushauri (RCC) ,Kunenge alitaka kujitathmini kwa wingi wa viwanda na tija ndani ya jamii kwenye ajira na kuinua mapato.
Alieleza kila Taasisi ina wajibu wa kujua matarajio ya Mkoa na Taifa ,Kwani haiwezekani kujivunia kuwa na viwanda vingi wakati havitoi ajira ya kutosha na haviongezi mapato.
“Tunajivunia kuwa na viwanda vingi, Lakini hakuna haja ya kuwa na viwanda vingi, Lakini haviendelei ,havina tija,vinakufa ,vinachechemea au havitoi ajira”
Vilevile alihimiza wananchi kujitokeza kuchanja chanjo ya Uviko19 kwani idadi ya watu 7,204 sawa na asilimia 28 ya waliyojikeza hadi Sasa hairidhishi .
Alisema ,chanjo ya Uviko19 alisema awali mkoa ulipokea chanjo 30,000 na awamu ya pili imepokelewa 25,000 Lakini idadi ya wanaojitokeza hairidhishi.
“Chanjo hii ni hiari lakini ifikie hatua tutumie busara na hekima,”alisema Kunenge .
Suala la migogoro ya ardhi, “:;Nimegundua watu hawafuati Sheria na kusababisha matatizo ya migogoro ya ardhi kukua , Watendaji upande wa mipango miji suluhisho katika kupanga miji sio kurasimisha ,badala yake muendeleze kupanga miji ili kupunguza migogoro hii ambayo inakuwa kutokana na kosa la kutojipanga toka kipindi cha nyuma “alibainisha Kunenge.
Sambamba na hayo Kunenge alieleza,mkoa umepokea Bilioni 13.9 fedha za Uviko19 kwa ajili ya miundombinu ya madarasa na afya.
Akichangia hoja mbalimbali katika kikao hicho Mbunge wa viti maalum mkoa wa Pwani,Subira Mgalu alishauri hatua zichukuliwe kwa wale ambao wanaonekana kujihusisha na upotevu wa dawa na kuomba uongozi wa mkoa kufuatilia suala hili ili liweze kukomeshwa.
Alisema, kwa taarifa ya Wizara ya afya zipo wilaya ambazo hospital za rufaa na vituo vya afya vinavyosababisha upotevu wa dawa na kupelekea kero kwa jamii hivyo kuna kila sababu ya kuliona hili.
Akichangia agenda ya vigezo vya baadhi ya wilaya kupanda kuwa Manispaa,Mgalu alisema vigezo visiwe sababu kwakuwa bado Kuna uhitaji ,kwa kuwa na umuhimu huu , wananchi wahimizwe kujitokeza katika zoezi la sensa ili kupata idadi kamili .
Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini , Michael Mwakamo alisema mkoa huo Ni mkoa mkongwe Lakini hauna Manispaa, viongozi wasiwe sehemu ya kuweka vikwazo na kukwamisha suala hili.
Alisema Kibaha Ni Kama Manispaa nyingine nchini ,vigezo vilivyopo viangaliwe ili kukidhi vigezo.
Sheikh mkuu wa mkoa wa Pwani, Hamis Mtupa alibainisha, mkoa wa Pwani unatakiwa upendeze na kuondoa dhana ya vigezo hali inayorudisha nyuma maendeleo ya Mkoa kwa miaka mingi.
Kwa upande wake mwanachama wa TCCIA Charles Zacharia ambae pia ni mwekezaji wa Masasi Food Industries aliomba wawekezaji wakutanishwe na mkoa ili kuweka mezani changamoto zao ili ziweze kufanyiwa kazi.
Zacharia alieleza, wao ndio wanajua changamoto zinazowasibu kwenye uzalishaji hivyo endapo wakikutana itawezesha kujua wapi wanakwama,nini kikwazo ili vitatuliwe.