Waziri wa Viwanda na Biashara Prof.Kitila Mkumbo,akizungumza na waandishi wa habari leo November 24,2021 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kuhusu hatua zilizochukuliwa katika upandaji bei wa vifaa vya ujenzi nchini.
………………………………………………………..
Na.Alex Sonna,Dodoma
WIZARA ya Viwanda na Biashara imetaja hatua tano zilizochukuliwa kwa ajili ya kupunguza makali ya kupanda kwa bei kwenye vifaa vya ujenzi nchini.
Hata hivyo, imesema kupanda kwa bei za saruji nchini si halali kwa kuwa hakuna gharama za uzalishaji zilizoongezeka kwa kipindi cha Septemba hadi Novemba 2021 na kuagiza Tume ya Ushindani (FCC) kufanya uchunguzi na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza leo November 24,2021 jijini Dodoma na waandishi wa habari Waziri wa Viwanda na Biashara Prof.Kitila Mkumbo amesema kwa tathmini iliyofanywa Septemba hadi Novemba mwaka 2021, kwenye mikoa tisa inayoongoza kwa matumizi ya vifaa vya ujenzi inaonesha kiwango cha ujenzi kimeongezeka na kufikia asilimia 14.
Amesema kuwa Wizara itaanza kutoa mwenendo wa bei ya bidhaa kwa wastani kila mwezi kwa mikoa yote nchini ili wananchi kupata uhalisia wa bei ya bidhaa hizo.
“Tume ya Ushindani(FCC) imehimizwa kuendelea kufuatilia kwa karibu upangaji wa bei nchini na kuchukua hatua stahiki kwa wafanyabiashara wanaokiuka sheria ya ushindani nchini ikiwamo kuzuia na kudhibiti wafanyabiashara kupanga bei ya pamoja kwa kuwa hawaruhusiwi,”amesema Prof.Mkumbo
Ametaja hatua ya tatu ni kujadiliana na Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira ili kurekebisha sheria na kanuni mbalimbali ili kuruhusu kuingizwa kwa malighafi zinazohitajika katika uzalishaji wa bidhaa za chuma ikiwamo vyuma chakavu kutokana na kutotosheleza.
Hata hivyo, alisema serikali imepiga marufuku uuzaji wa shaba chakavu nje ya nchi ambazo hutumika kuzalisha bidhaa za vyuma.
“Tunatarajia Desemba bei itashuka kutokana na kupiga marufuku, na hatua ya mwisho ni kuzalisha chuma chetu nchini ambapo serikali ina mpango wa kutekeleza miradi kielelezo ya kuwezesha kuzalisha chuma ya kutosha nchini, kwa ajili ya viwanda vyetu nchini,”amesisitiza
Kuhusu bidhaa ya saruji, Waziri Mkumbo alisema Wizara imebaini kupanda kwa kiwango kidogo cha bei ya bidhaa hiyo kunasababishwa na mfumo wa usambazaji na si gharama za uzalishaji.
“Wauzaji hawakuwa na sababu yeyote ya kupandisha bei ya saruji kwa kuwa hakuna kilichoongezeja, hivyo upandaji huu sio halali.”
“Wizara hufanya tathmini ya mara kwa mara ya mwenendo wa uzalishaji, usambazaji na bei ya bidhaa muhimu ikiwamo vyakula na vifaa vya ujenzi,”amesema
Pia amesema kuwa bidhaa nyingi za ujenzi zinazalishwa nchini kwasasa ambapo kuna viwanda tisa vinavyofanya kazi ya kuzalisha saruji.
“Kuna kiwanda cha Maweni kule Tanga ambacho kitaanza kuzalisha saruji, na taarifa zinaonesha kuwa kwasasa tunazalisha tani milioni tisa za saruji kwa mwaka ambazo zinatosheleza mahitaji,”amesema
Aidha amesema kuwa katika mwenendo wa bei waliofuatilia kwa kipindi cha Septemba hadi Novemba bei za saruji nchini kwa mikoa tisa iliyofanyiwa tathmini ambayo ndio wazalishaji wakubwa wa saruji, bei imepanda kwa wastani wa Sh.1000.
“Mfano mkoa wa Mwanza bei za saruji zimeongezeka kutoka Sh.19,000 hadi 20,000 kwa mfuko wa kilogramu 50, Dar es salaam kutoka Sh.14,000 hadi 15,000.”
“Kuna mikoa bei imepungua kwa mfano Ruvuma bei imeshuka kwa asilimia 15 kutoka Sh.17,000 kwa mwezi Septemba hadi Sh.14,500 kwa Novemba 2021, kwasababu kiwanda cha Dangote kimerejesha uzalishaji kwa mwezi Oktoba,”amesema
Kuhusu mabati, Prof.Mkumbo amesema uwezo uliopo kwenye viwanda vilivyopo ni kuzalisha mabati milioni 14 kwa mwaka na bei imepanda kwa wastani wa asilimia 5.5 kwa kipindi cha Septemba hadi Novemba mwaka 2021.
“Kwa mfano Mwanza imepanda bei kutoka Sh.31,700 hadi 33,400, kwa Dar es salaam kutoka Sh.28,000 hadi 29,000,”ameeleza
KUuhusu nondo, Prof.Mkumbo amesema katika viwanda 16 vilivyopo nchini vinazalisha tani 750,000 na kwa tathmini iliyofanywa bei imeongezeka kwa asilimia sita.
“Mwanza nondo za milimita 12 zilipanda kutoka Sh.44,000 hadi 47,500, huku Dar es salaam ilikuwa Sh.41,600 hadi 43,700,”amesema.
Hata hivyo amesema sababu za kupanda kwa bidhaa za chuma zinatokana na gharama za uzalishaji kwa kuwa bidhaa nyingi zinaagizwa kutoka nje.
“Viwanda vingi vya nondo vinahangaika kutafuta malighafi kwa kuwa zinategemea vyuma chakavu, tathmini inaonesha bidhaa hizi kupanda bei hakutokani na mfumo wa usambazaji bali inatokana na gharama za uzalishaji,”amesema