Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Mhe. Jamali Kassim Ali akizungumza na Waandishi wa Habari pamoja na Wafanyakazi waliopo chini ya Wizara hiyo, kuhusu mafanikio ya Mwaka mmoja katika Uongozi wa awamu ya nane, ndani ya Wizara yake, hafla iliyofanyika Ukumbi wa ZRB Mazizini Mjini Zanzibar.
Baadhi ya Waandishi wa habari na Wafanyakazi waliopo chini ya Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, wakimsikiliza Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Jamali Kassim Ali (hayupo pichani), wakati akielezea mafanikio ya Mwaka mmoja katika Uongozi wa awamu ya nane. Ndani ya Wizara yake, hafla iliyofanyika Ukumbi wa ZRB Mazizini Mjini Zanzibar.
Picha na Maryam Kidiko / Maelezo Zanzibar.
………………………………………………..
Na Kijakazi Abdalla ,Maelezo
Wizara ya Nchi,Ofisi ya Rais,Fedha na Mipango kwa kipindi cha Novemba 2020 mpaka Septemba 2021 imekusanya Tzs 710.84 Bilioni sawa na asilimia 69 ya makadirio ya kukusanya Tzs 1,023.56 Bilioni.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar Jamal Kassim Ali huko Ukumbi wa Bodi ya Mapato Mazizini(ZRB) katika kikao cha mafanikio ya Mwaka mmoja wa awamu ya nane.
Amesema makusanyo hayo ni ongezeko la asilimia 24 ikilinganishwa na makusanyo ya Tzs 572.61 Bilioni zilizokusanywa kwa kipindi cha mwezi Novrmba 2019 mpaka Septemba 2020.
Aidha amesema miongoni mwa sababu zilizopelekea kuongezeka kwa mapato ni mfumo ya kielektronik ambayo imeunganishwa serikalini na kwa wafanyabiashara.
Amesema mifumo hiyo ni ZanMalipo ambayo inadhibiti upotevu wa mapato ya Serikali pamoja na kupata taarifa sahihi na kwa wakati.
Akizungumzia mafanikio ya mwaka mmoja ya Serikali ya awamu ya nane Waziri Jamali amesema hali ya ukuaji wa uchumi imeimarika Zanzibar na imefikia wastani wa asilimia 2.2 kwa robo ya kwanza.
Amesema hali hiyo inatarajiwa kuimarika kutokana kwa kupungua kwa maambukizi ya maradhi ya Uviko 19 duniani na kuwepo hali ya amani na utulivu hali ambayo itaendelea kuimarika kwa uchumi.
Aidha amesema pato la taifa limeongezeka na kufikia Tzs 3.116 Bilioni kwa mwaka 2020 na pato la mwananchi kufikia Tzs 2.526 Milioni sawa na Dola za kimarekani 1,099.
Amesema kutokana na hali hiyo Waziri Jamal amesema kwa mujibu wa vigezo vya kimataifa kipato cha mwananchi Zanzibar kinaifanya Zanzibar kuwa nchi ya uchumi wa kipato cha kati kuvuka kiwango cha dola za kimarekani 1.040 kilichowekwa kimataifa.
Hata hivyo amesema katika kusimamia ukusanyaji wa mapato ya Serikali kutokana na vyanzo vya ndani na nje ya nchi kwa kipindi cha Novemba 2020 mpaka Septemba 2021 Wizara ya Fedha na Mipango imeweza kukusanya Tzs710.84 Bilioni sawa na asilimia 69 ya makadirio ya kukusanya Tzs.1Bilioni.