Afisa Sera na Majadiliano wa TFCG Elida Fundi akizungumza kwenye mkutano huo.
Picha ya pamoja baada ya mkutano huo.
Picha ya pamoja Bwala la Hokororo.
………………………………………………
MRADI wa Kuhifadhi Misitu kupitia biashara Endelevu ya mazao ya misitu unaotekelezwa na Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu
(MJUMITA) kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo na Ushirikiano la Uswis (SDC) umewabadilisha wananchi wa Kijiji cha Nambinda wilayani Liwale mkoani Lindi na sasa wameacha tabia ya kuhalibu misitu na wamejua thamani yake.
Wananchi wa Kijiji hicho wameanza kujua thamani ya misitu baada ya mashirika hayo kuwapa elimu ya ya shughuli za uzalishaji endelevu wa mazao yatokanayo na misitu na matumizi bora ya ardhi.
Mzalishaji wa mbao wa kijiji hicho Hemed Kipaga akizungumza kwa niaba ya wenzake wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari ambao wapo katika ziara ya kujifunza kuhusu utekelezaji wa Usimamizi Shirikishi wa Misitu wilayani Liwale mkoani hapa waliotaka kujua hali ya utunzaji wa misitu ilivyokuwa kabla ya kupokea mradi huo alisema ilikuwa mbaya sana.
“Kwanza kabisa napenda kuyashukuru mashirika haya TFCG na MJUMITA kwa kutuletea mradi huu kwani tumeweza kufanikiwa mambo mengi, kabla ya mradi hatukuwa na matumizi bora ya ardhi ukataji wa miti ulikuwa wa hovyo hovyo tu mtu alipokuwa akijisia alikuwa akiingia msituni na kukata miti” alisema Kipaga.
Alisema baada ya kupata mradi huo wameweza kutenga maeeneo ya matumizi bora ya ardhi ambayo aliyataja kuwa ni ya makazi msongamano,eneo la kilimo na la kuhifadhi msitu na kuwa mpango huo umesaidia sana kuhifadhi misitu.
Awali akizungumza na waaandishi wa habari Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Liwale, Tina Sekambo alisema halmashauri hiyo imetenga sh.30 milioni kwa ajili ya kusaidia utunzaji wa misitu na kuwa mabadiliko ya kiuchumi yamekuwa ni moja ya sababu ya wananchi katika baadhi ya maeneo ya wilaya hiyo kukata miti ya asili na kuanza kupanda mikorosho.
Mkuu wa Wilaya ya Liwale Judith Nguli alisema utunzaji wa miti ni jukumu la kila mwananchi na alitumia nafasi hiyo kuwaomba wadau mbalimbali kufika katika wilaya hiyo kusaidia utunzaji wa misitu na kuwa mtu yeyote atakaye bainika akihalibu misitu kwa namna yoyote atachukuliwa hatua za kisheria.
Nguli aliyashukuru mashirika yanayoisaidia serikali katika suala zima la uhifadhi wa misitu ya asili katika wilaya hiyo.