Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Daniel Chongolo akisalimiana na Viongozi wa Shina na Serikali wakati akiwasili katika shina namba 6 Majengo, Kasulu mkoani Kigoma ikiwa sehemu ya ziara yake katika kuimarisha uhai wa chama katika ngazi ya Mashina. (Picha na CCM Makao Makuu)
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndg. Daniel Chongolo amezitaka kamati za ulinzi na usalama katika Wilaya na Mikoa kuwatumia wenyeviti wa mashina (Mabalozi) wa mashina katika kutambua wahalifu na wahamiaji haramu wanaoingia na kutishia amani na usalama katika maeneo yao.
Katibu Mkuu Ndg. Chongolo amesema, Mabalozi wa Mashina wanakuwa na taarifa za kutosha na uhakika kuhusu wahusika halali wa maeneo yao na wasio wahusika kuanzia ngazi ya mashina mpaka Wilaya.
Katibu Mkuu amesema hayo tarehe 18 Novemba, 2021 wakati akizungumza na wananchi pamoja na wanachama wa CCM katika shina namba sita la Kata ya Nyamidaho wilaya ya Kasulu ambapo akiambatana na Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa amefika mkoani Kigoma Kwa ziara ya siku mbili kukagua uhai wa chama na utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025.
Amesema kuwa mabalozi hao kupitia vikao vyao vya mashina wanaweza kusaidia katika kupata taarifa sahihi katika kupanga mipango ya maendeleo ya Wilaya na mikoa Kwa sababu wanakuwa na taarifa zote kuhusu idadi ya watu wakazi katika mashina yao Kwa ujumla, idadi ya wanafunzi wanaosoma na wasio soma katika maeneo yao, wakulima na baadhi ya watu wasiokuwa na shughuli yoyote katika maeneo yao.
Katibu Mkuu ametoa kauli hiyo baada ya Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Kanali I. A. Mwakisu kueleza kuhusu uwepo wa mamia ya wahamiaji haramu kutoka Burundi kuingia katika Wilaya hiyo na kuanza kujihusisha na shughuli mbalimbali ikwemo Kulima mashamba ya watanzania ndani ya Wilaya hiyo.
“Idara ya Uhamiaji imekuwa ikikamata wahamiaji haramu wakiwa nchini bila kibali. Tatizo hili ni kubwa Sana kwani mamia ya wahamiaji haramu kutoka Burundi ndio wanaolima mashamba ya watanzania wengi ndani ya Wilaya ya Kasulu,” ameeleza Mkuu wa wilaya.