Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiongea na Balozi wa Korea Kaskazini nchini Mhe. Kim Yong Su katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
Balozi wa Korea Kaskazini hapa nchini Mhe. Kim Yong Su akimuelezea jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula walipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
Mkutano wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Balozi wa Korea Kaskazini hapa nchini Mhe. Kim Yong Su ukiendelea katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula katika picha ya pamoja na Balozi wa Korea Kaskazini hapa nchini Mhe. Kim Yong Su mara baada ya kumaliza mkutano wao leo katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akizungumza na Mwakilishi wa Heshima wa Kazakhstan nchini Tanzania Bw. Ameir Nahdi katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam
Mwakilishi wa Heshima wa Kazakhstan nchini Tanzania Bw. Ameir Nahdi akiongea na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula wakati walipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam
*****************************
Na Mwandishi wetu, Dar
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea (DPRK) zimekubaliana kuimarisha misingi ya uhusiano wa kidiplomasia baina ya mataifa hayo kwa maslahi mapana ya pande zote mbili.
Ahadi hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula pamoja na Balozi wa Korea Kaskazini mhe. Kim Yong Su walipokutana leo kwa mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
Waziri Mulamula amesema Tanzania na Korea Kaskazini zitaendelea kushikiana katika kuimarisha zaidi misingi ya uhusiano baina ya nchi hizo kwa kuzingatia Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania.
“Nimemhakikishia Balozi wa Korea Kaskazini kuwa sisi misingi yetu ya Sera ya Mambo ya Nje (Tanzania) haijabadilika iko vilevile, na tutaendelea kuimarisha uhusiano wetu, amesema Waziri Mulamula.
Kwa upande wake Balozi wa Korea Kaskazini hapa nchini, Mhe. Kim Yong Su amesema kuwa Korea na Tanzani ni marafiki wa muda mrefu na kwa mkutano wetu tumejadili namna ya kuboresha uhusiano wetu wa kidiplomasia.
Balozi Kim Yong Su amesema kuwa pamoja na mambo mengine wamekubaliana kuboresha uhusiano wa kidiploasia kwa maslahi ya pande zote mbili.
“Ushirikiano wa Korea Kusini na Tanzania ni mzuri na imara ………. naahidi kuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea itaendelea kushirikiana na Tanzania kiutamaduni, kisiasa, kiuchumi, ulinzi na kilimo hii ikiwa ni jitihada za kuimarisha ushirikiano wetu kwa maslahi ya mataifa yetu,” amesema Balozi Su.
Balozi Su ameongeza kuwa Korea Kaskazini inapongeza jitihada mbalimbali ambazo zimekuwa zikichukuliwa na Tanzania katika kuhakikisha inasonga mbele kimaendeleo katika nyanja za kiuchumi pamoja na kuimarisha/kuboresha diplomasia na mataifa mengine duniani.
“Nampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada mbalimbali anazaochukua katika kuimarisha uchumi wa Tanzania na wananchi wake pamoja na kidiplomasia,” ameongeza Balozi Su.
Tanzania na Korea Kaskazini zilianzisha uhusiano wa kidiplomasia Aprili, 1992, ambapo nchi hizi zimekuwa zikishirikiana kidiplomasia katika sekta ya elimu, afya, sayansi na utamaduni pamoja na utalii.
Katika tukio jingine, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi wa Heshima wa Kazakhstan nchini Tanzania Bw. Ameir Nahdi ambapo viongozi hao wajejadili masuala mbalimbali ikiwemo za biashara na uwekezaji katika sekta za mafuta na gesi, kilimo pamoja na uchimbaji na uchakataji wa madini na utalii.