Mwandishi Wetu
Dar es Salaam. Maandalizi ya mashindano ya kimataifa ya urembo ya Miss East Africa 2021 yako katika hatua za mwisho ambapo tayari nchi zinazoshiriki katika mashindano hayo zimeshatuma wawakilishi wake.
Makamu wa Rais wa mashindano hayo, Jolly Mutesi alisema washiriki hao kwa sasa wapo katika maandalizi ya mashindano hayo makubwa katika ukanda huu wa AfriKa.
Alisema Nchi zilizokwisha tangaza wawakilishi wake ni pamoja na Kenya, Uganda, Rwanda, South Sudan na Somalia huku zingine ni Reunion, Ethiopia, Malawi, Burundi na Mauritius.
“Tanzania itawakilishwa na Mrembo Queen Mugesi ambae aliwashinda warembo zaidi ya 2,600 wa Tanzania walioomba kuiwakilisha nchi kwa njia ya mtandao ambapo Queen Mugesi alichaguliwa katika mchakato ulioendeshwa na wataalamu wa mambo ya urembo kwa zaidi ya mwezi mmoja.
“Warembo wanaoshiriki katika mashindano hayo wanatarajiwa kuanza kuwasili Novemba 26, 2021 na fainali ya mashindano hayo itafanyika tarehe Desemba 17, 2021 katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es salaam kuanzia saa 12 jioni,” alisema.
Alisema, mashindano ya Miss East Africa ambayo yaliasisiwa na Mtanzania Rena Callist mwaka 1996, yanasubiriwa kwa hamu kubwa na wapenzi wa mambo ya urembo na yanatarajiwa kuangaliwa na zaidi ya watu milioni 200 moja kwa moja LIVE kupitia katika television na wengine wengi zaidi wataangalia kupitia Internet duniani kote.
Alisema Mashindano ya Miss East Africa yanaandaliwa na kampuni ya Rena Events LTD ya jijini Dar es salaam.