NA MUSSA YUSUPH,MISSENYI
RAIS Samia Suluhu Haasan ametoa zaidi ya sh. bilioni 500 kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika Mkoa wa Kagera ambapo mkoa huo umeshika nafasi ya tatu kitaifa kwa kupatiwa fedha nyingi za maendeleo.
Katika fedha hizo, sh. bilioni 2.7 Rais Samia amezitoa kujenga madarasa ya shule za sekondari na shule 10 mpya shikizi zilizopo Wilaya ya Missenyi, Mkoa wa Kagera.
Aidha, kupitia fedha za tozo za miamala ya simu, Rais Samia ametoa sh. milioni 250 zilizotumika kujenga Kituo cha Afya Kanyigo huku kiasi kingine cha fedha kama hizo zikitarajiwa kutolewa kujenga Kituo cha Afya Kakunyu.
Hayo yalielezwa na Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Christina Mndeme, wakati aliposhiriki kikao cha Shina Namba tatu, Tawi la CCM Nsunga, Kata ya Nsunga, Wilaya ya Missenyi, Mkoa wa Kagera.
“Rais wetu ni msikivu aliposikia kilio cha ukubwa wa tozo, alipunguza lakini kile kilichobaki kinaletwa kwenu kuwaletea wananchi maendeleo. Tuendelee kumuunga mkono Rais wetu Samia Suluhu Hassan.
Aliongeza kuwa: ”Tunapaswa kusimamia utekelezaji wa ilani ya CCM kwa kukagua miradi inayotekelezwa, utengaji wa bajeti na wakati wa ukaguzi wa miradi hiyo mabalozi na kamati zao za uongozi washiriki kukagua miradi husika iliyopo katika mashina yao.
Pia, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara, alisema mabalozi washirikishwe katika kuandaa mipango ya bajeti ili kufahamu mahitaji ya wananchi na kutoa mchango wa mawazo kuhusu miradi itakayotekelezwa.
Kuhusu uchaguzi wa ndani ya chama utakaofanyika mwakani, aliwataka mabalozi kuzingatia kigezo cha wagombea kushiriki vikao vya mashina.
“Watakaoomba nafasi ndani ya chama au kugombea kwenye dola, muangalie wamehudhuria mikutano mingapi ya shina. Tunataka tujenge nidhamu na uwajibikaji kwenye mashina. Ilani inatuelekeza kuhudhuria mikutano, je kiongozi anahudhuria mikutano mingapi na sio kuomba udhuru,” alisisitiza.
Vilevile, aliwataka wanachama wenye nia ya kugombea uongozi ndani ya chama kuacha kupanga safu kwani muda wa kufanya hivyo bado haujawadia.
“Tuache kupitapita, tujiepusha kupanga safu, fitina na kuchafuana. Wakati ukifika kila mtu mwanachama halali anapaswa kugombea, lakini sio sasa hivi tuwaache viongozi wafanye kazi,” alisema.
Aliwaomba mabalozi wa mashina kuendelea kutoa hamasa kwa wananchi kupata chanjo ya Uviko-19 pamoja na kushiriki Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika mwakani.