*********************
Nteghenjwa Hosseah, Arusha
Naibu Katibu Mkuu anayesghulikia Afya Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dkt. Grace Magembe amewataka Watanzania kufanya mazoezi kuwa sehemu ya maisha yao ili kuweza kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.
Dkt. Grace ameyasema hayo wakati akifunga Kongamano la 3 la Kisayansi la magonjwa yasiyoambukiza likilofanyika kwenye Ukumbi wa AICC Jijini Arusha.
Akizungumza katika Kongamano hiko Dkt. Grace amesema kila mtu akifanya mazoezi kuwa sehemu ya maisha yake atajikinga kwa asilimia kubwa na magonjwa yasiyoambukiza.
“Mtindo wa maisha tunaoishi ndio unachangia kwa kiasi kubwa magonjwa yasiyoambukiza ambayo yanauwa watu wengi na kwa kuwa tunakaa muda mrefu, tunatumia magari kila tunapoenda na tunakula vyakula vyenye sukari na mafuta kwa tabia hii magonjwa haya yatatushambulia tu.
Tunachoweza kufanya ni kutumia mazingira yako kufanya mazoezi ukiwa nyumbani tenga muda kidogo fanya mazoezi, ukitoka kazini achana na gari tembea, umesafiri beba kamba yako ruka ukiwa hotelini, kwa siku ukitumia hata nusu saa inatosha kabisa kuimarisha miili yetu” alisema Dkt. Grace.
Pia alihamasisha watanzania kuwa na tabia ya kupima afya zetu mara kwa mara ili kama kuna changamoto yeyote ya afya iweze kutubiwa mapema kuliko kusubiria mpaka uanze kuumwa.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Kongamano la Kisayansi Prof. Appolinary Kamuhabwa amesema katika Kongamano la 3 la Kitaifa la magonjwa yasioambukiza
jumla ya mada 168 zimewasilishwa huku 96 zikiwasilishwa kwa mdomo na 72 kwa mabandiko.
Dhima Kuu ya Kongamano hili ni Uhusishwaji na Ushirikishwaji wa Sekta anuai katika kudhibiti magonjwa yasioambukiza na jumla ya Taasisi 24 zimeshiriki.
Maadhimisho ya wiki ya magonjwa yasiyoambukiza ambayo kitaifa yamefanyika Arusha kuanzia Novemba 6 hadi 13 mwaka huu,Mkuu wa Mkoa Arusha John Mongela alisema kutokana na takwimu hizo kuna haja ya kila mtu kuchukua hatua ya kukabiliana na magonjwa hayo