Meya Manispaa ya Mpanda Haidary Sumri
Baadhi ya wajumbe waliohudhuria katika kikao hicho sensa ya watu na makazi.
………………………………….
Na Zillipa Joseph, Katavi
Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi imezindua kamati za kusimamia Sensa ya Watu na Makazi kwa ngazi ya wilaya hadi ngazi ya kitongoji.
Akizindua kamati hizo, Mwenyekiti wa kamati ambaye ni mkuu wa wilaya ya Mpanda Jamila Yusuph amewataka wanakamati kuhakikisha wanatoa elimu katika jamii juu ya umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi bila kuacha kundi lolote.
“Hizi Kamati, kila mmoja akatimize wajibu wake, muda ni mfupi wa kuanza maandalizi na tujue tunaanza maandalizi haya ya Sensa kama tulivyoambiwa kuna vipindi vitatu, tuko kwenye awamu ya kwanza, ambayo watu wengi kipindi hiki wako mashambani, sasa hivi tuna kazi kubwa ya kushughulika na hawa watu ambao watakuwa wameenda mashambani wapate elimu juu ya hii sensa” alisisitiza DC Jamila Yusuph.
Awali akiwasilisha taarifa ya uundwaji kamati hizo, Kaimu Katibu Tawala Wilaya ya Mpanda Keneth Pesambili amesema Sensa ya Watu na Makazi ni utaratibu wa kukusanya, kuchambua, kutathmini, kuchapisha na kusambaza takwimu za kijiografia, kiuchumi na Kijamii zinazohusu watu na makazi katika nchi kwa kipindi maalumu.
Amesema taarifa za kila mtu zitachukuliwa zoezi litakapomkuta na kuwaondoa hofu wale watakaokutwa mbali na maeneo yao ya makazi na kuongeza kuwa Sensa ya Watu na Makazi inayahusu makundi yote ya watu bila kujali umri na jinsia zikiwemo mali kama nyumba, mifugo n.k
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa manispaa ya Mpanda, Haidary Sumry amesisitiza elimu kutolewa katika jamii ili watu waondokane na dhana potofu kuwa kuhesabiwa ni ushirikina.
Aliwaomba wananchi kutowaficha watu wenye ulemavu kwani ni haki yao kuhesabiwa ili serikali ipate idadi kamili.
“Tuondoe zile dhana, maana sensa za huko nyuma kuna mambo ya kiimani yaliingia, yakawa yanazuia watu wao wasihesabiwe, lakini tunajua kuna makabila fulani wakawa wanaona kuhesabiwa labda ni kudaiwa kodi au vitu vingine kama hivyo” alisema Sumry
“Lakini zaidi kwa sisi wanasiasa, hili zoezi sio la kisiasa ni zoezi ambalo linatamani kujua idadi ya wananchi na wakazi tulionao lakini kwa wale wenye familia, huko nyuma pia kuna watu walikuwa na Watu wenye Ulemavu badala ya kutoa takwimu sahihi walizificha” Alisisitiza.
Baadhi ya wajumbe katika kikao hicho wameitaka jamii kutoa taarifa za kweli kwa kuwa hiyo ni faida kwa eneo husika pale serikali inapotaka kupeleka maendeleo kwa kuwa idadi ya watu au mifugo ndicho kigezo kikubwa cha ushawishi.
Sensa ya Watu na Makazi nchini Tanzania inatarajiwa kufanyika Agosti mwaka 2022.