Na Calista Nyimbo, Morogoro.
WAJUMBE wa Kamati ya Ukaguzi Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wamekumbushwa kufuata sheria, taratibu na miongozo inayotolewa ya kamati hiyo ili kuboresha ufanisi wa kazi na kutimiza malengo ya chuo.
Hayo yamesemwa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Profesa. Raphael Chibunda wakati akifungua mafunzo ya Siku mbili kwa kamati ya Ukaguzi wa ndani ya Chuo iliyofanyika ukumbi wa Kituo cha kuratibu hewa ya ukaa Katika Kampasi ya Edward Moringe Morogoro.
“Mimi ninamatumaini makubwa sisi sote tunaoshiriki mafunzo haya tutakuwa wasikivu na tutajipa muda ili kuelewa na kukubali kukumbushwa majukumu na umuhimu wa shughuli za ukaguzi katika kusimamia majukumu ya Chuo” alisema Profesa. Chibunda.
Chibunda alisema kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango kazi wa Kamati ya Ukaguzi ya mwaka wa fedha 2021/2022 na ni sehemu ya kutekeleza hati idhini ya kamati kuwa yatolewe mafunzo mafupi kwa wanakamati wa kamati ya ukaguzi.
“kama wengi wetu tunavyofahamu Kamati hii ndio jicho la Baraza katika usimamizi kuhakikisha kwamba utendaji wetu unazingatia kanuni, taratibu, sera, mifumo na miongozo mbalimbali ya kiserikali na ile ambayo inatolewa na baraza letu la chuo” alisema Chibunda.
Pia ameelezea dhumuni la mafunzo hayo kuwa ni kuwaongezea uwelewa kamati ya ukaguzi na kuwakumbusha majukumu yao na umuhimu wa kamati ya ukaguzi katika kushauri baraza la chuo kwenye utekelezaji wa majukumu yao hususani katika usimamizi wa chuo.
Aidha aliongeza kuwa mafunzo hayo yalihusisha pia Menejimenti ya chuo kutokana na Kamati ya ukaguzi kufanyakazi karibu na menejimenti hiyo hivyo mafunzo hayo yatawasaidia wote kuelewa masuala muhimu ya usimamizi wa rasilimali za chuo na kujiandaa na viatalishi mbalimbali vinavyoikabili chuo hicho.
Mtoa mada katika mafunzo hayo ambaye ni Muasisi wa Taasisi ya Ukaguzi wa ndani (TIA) Godfrey Kilenga ameshukuru kwa mualiko alioupata kutoka SUA kutoa mafunzo hayo na kwamba ana imani yataleta mabadiliko makubwa chuoni hapo.
Alisema kuwa miongozo mingi ya shughuli za ukaguzi zinatoka serikali hivyo ni vizuri wajumbe hao kufanyia kazi yatakayofundishwa ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kutimiza malengo waliyojiekea.