Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Bw. Denis Bandisa akizungumza mjini Sumbawanga kuhusu utayari wa halmashauri za Rukwa kushirikiana na RITA kufanikisha zoezi la usajili wa watoto wenye umri chini ya miaka mitano zoezi litalofanyika kwa wiki mbili kuanzia leo.Bi. Emmy Hudson Kaimu Kabidhi Wasii Mkuu na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) akitoa maelezo kuhusu Mpango wa Usajili wa Watoto wa Umri chini ya Miaka Mitano kwenye semina ya viongozi iliyofanyika leo mkoani Rukwa,Sumbawanga.
Mwakilishi wa UNICEF nchini anayeshugulikia Masuala ya Ulinzi wa Watoto Bi. Gillian San Aye akizungumza kwenye semina ya viongozi wa mkoa wa Rukwa kuhusu mpango wa usajili wa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ambapo amesema UNICEF itashirikiana na Tanzania kufanikisha zoezi hilo.
Bw. Rashid Maftah kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Dodoma akizungumza kuhusu umuhimu wa Halmashauri za Mkoa wa Rukwa kutoa ushirikiano kwa RITA ili kuwezesha usajili wa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ufanikiwe na kuwa endelevu .Ametoa wito huo leo mjini Sumbawanga kwenye semina ya viongozi wa mkoa na wilaya iliyoratibiwa na RITA.
Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Bw. Denis Bandisa akizungumza mjini Sumbawanga kuhusu utayari wa halmashauri za Rukwa kushirikiana na RITA kufanikisha zoezi la usajili wa watoto wenye umri chini ya miaka mitano zoezi litalofanyika kwa wiki mbili kuanzia leo.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Joseph Mkirikiti (katikati waliokaa) akiwa kwenye picha ya pamoja na Maafisa wa Sekretariati ya Mkoa leo mara baada ya semina ya viongozi kuhusu Mpango wa Usajili wa Watoto Walio na Umri Chini ya Miaka Mitano utakaofanyika kote mkoani Rukwa hivi karibuni chini ya RITA.
****************************
Mkoa wa Rukwa unakadiriwa kuwa watoto wenye umri wa miaka chini ya miaka mitano wapatao 264,068 huku waliosajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa ni asilimia tano pekee katika mwaka 2021.
Akizungumzia hilo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joseph Mkirikiti ameeleza kutoridhishwa kwake na takwimu hizi huku akisisitiza kuwa kushindwa kusajili watoto wanaozaliwa katika kaya kunakwamisha upangaji wa mipango ya maendeleo ya mkoa na taifa.
“Hivyo ni matumaini yangu kuwa mpango huu wa usajili wa watoto wa umri chini ya miaka mitano (U5BRI) utawezesha mabadiliko chanya na ni lazima tuhakikishe kila mtoto anayestahili anapata huduma bila usumbufu,” alisisitiza.
Mkirikiti alitoa kauli hiyo leo (02.11.2021) wakati akifungua semina ya viongozi wa wilaya na mkoa kuhusu Mpango wa Usajili wa Watoto wa umri chini ya miaka mitano (Underfive Birth Registration Initiative-U5BRI) iliyofanyika katika Mji wa Sumbawanga ikiratibiwa na Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA).
Alisisitiza kuwa umuhimu wa cheti cha kuzaliwa ni mkubwa sana kwa wananchi ambao wanavihitaji kama uthibitisho wa umri na taarifa mbalimbali wakati wa kupatiwa huduma kama za elimu, afya na ajira.
“Kumekuwa na tabia ya wananchi kufatilia vyeti mara kinapohitajika hivyo kusababisha mlundikano mkubwa katika Ofisi za RITA wakati wa mazoezi maalumu. Tuwahimize wananchi wote walio na watoto wa umri huu na wana sifa stahiki kutumia fursa hii na wakishavipata wavitunze vizuri mahali salama kwani matumizi yake ni endelevu” alieleza.
Mkuu huyo wa Mkoa alitoa wito kwa waratatibu wa zoezi hilo RITA ,uhamiaji, NIDA na Ofisi ya Rais TAMISEMI kuwa makini na usajili wa watu hususan kwenye mkoa wa Rukwa ambapo unapakana na nchi za DRC na Zambia ili kuepusha usajili wa wasio raia..
“Uadilifu na uzalendo ni suala la muhimu wakati wa utekelezaji wa kazi hii. Vyombo vya Usalama mpo mkalisimamie hilo kwa kipindi chote kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi yetu alisisitiza Mkirikiti.
Kwa upande wake, Kaimu Kabidhi Wasii Mkuu na Mtendaji Mkuu wa RITA Emmy Hudson alisema kwa mujibu wa sensa ya watu na Makazi ya mwaka 2012 kwa mkoa wa Rukwa ni asilimia tano (5) tu ndio wamesajiliwa na kuwa na vyeti hivyo kwa zoezi litakaloanza limelenga kuhakikisha watoto wote wasio na vyeti vya kuzaliwa wanasajiliwa.
Kuhusu changamoto ya wahamiaji kutokana na Mkoa wa Rukwa kupakana na nchi jirani , Hudson alisema tayari wanashirikina na Idara zingine za serikali kudhibiti watu wasio raia kusajiliwa kwa mujibu wa sheria.
” Hivyo inawezekana wengine walikuja na watoto wa umri chini ya miaka mitano ambapo kwa mujibu wa Sheria ya Usajili wa Vizazi na Vifo, Sura ya 108 , watoto hao hawastahili kusajiliwa kwani wamezaliwa nje ya mipaka ya Tanzania” alisititiza .
Naye Meneja Utambuzi wa watu na Usajili toka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Julien Mafuru alisema watahakikisha watoto wanaosajiliwa ni wale tu wenye sifa za uraia na kuwa tahadhali zote zimechukuliwa kwa halmashauri za mkoa wa Rukwa.
Aidha Hudson alitumia fursa hiyo kunawashukuru wadau wa maendeleo ambao wanashirikiana na Serikali katika utekelezaji wa mpango huo ambao ni Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF), Serikali ya Canada kupitia Idara ya Mambo ya Nje, Biashara na Maendeleo (DFATD) na Kampuni ya Simu za Mkononi (TIGO).