**************************
Na Mwandishi Wetu, Morogoro
Michezo ya Nusu Fainali ya michuano ya Shirikisho la Michezo kwa Idara na Wizara za Serikali (SHIMIWI) imefanyika Oktoba 31, 2021 kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro ikihusisha michezo ya mpira wa netiboli, mpira wa miguu pamoja na mchezo wa kuvuta kamaba wanaume na wanawake.
Nusu fainali ya kwanza kuchezwa ni mchezo wa kamba wanaume na wanawake ambapo timu za wanaume za Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) na Idara ya Mahakama zimefuzu hatua ya fainali katika mchezo wa kuvuta kamba baada ya kuwavuta wapinzani wao kwenye mchezo wa nusu fainali uliofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani hapa.
Katika ubora wao kwenye mashindano hayo, Sekta ya Uchukuzi wamewavuta Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi kwa mivuto 2-0 huku Idara ya Mahakama wakiwavuta Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mivuto 2-0.
Kwa upande wa wanawake wa mchezo wa kuvuta kamba timu za Idara ya Mahakama na Ofisi ya Katibu Tawala mkoa wa Iringa (RAS Iringa) zimetinga fainali baada ya kuwashinda wapinzani wao ambapo RAS Iringa waliwavuta timu ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa 2-1 huku Idara ya Mahakama waliwavuta timu ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa 2-0.
Nusu fainali nyingine ambayo imechezwa kwenye mashindano hayo katika kiwanja cha Jamhuri Maniaspaa ya Morogoro, timu ya Ofisi ya Rais Ikulu wameshinda kwa kuwafunga timu ya Hazina kwa magoli 72-13 katika nusu fainali ya kwanza ya mchezo wa netiboli huku nusu fainali ya pili ikichezwa kati ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ambao waliifunga timu ya Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo kwa magoli 74-27 katika mchezo mwingine wa nusu fainali. Hivyo, katika mchezo wa fainali timu ya Ikulu itakutana na NAOT.
Katika mchezo wa soka timu ya Wizara ya Katiba na Sheria wameingia fainali baada ya kuwafunga Wizara ya Nishati kwa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali huku timu ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) nao wamekata tiketi ya kucheza hatua hiyo kwa kuifunga timu ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) kwa magoli 5-1 ambapo sasa watacheza fainali na Wizara ya Katiba na Sheria.
Michuano hii inayotarajia kufikia tamati Novemba 02, 2021 ambapo michezo hiyo itaendelea kesho kwa mechi za kutafuta mshindi wa tatu kwa michezo ya soka, netiboli na kuvuta kamba kwa wanawake na wanaume.