Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako (Mb) akizungumza na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) Kate Somvongsri alipofika Ofisini kwa Waziri leo Oktoba 28, 2021 jijini Dodoma kujitambulisha.
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) Kate Somvongsri akimkabidhi Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako (Mb) nyaraka za Mradi wa Jifunze Uelewe alipofika Ofisini kwa Waziri jijini Dodoma kujitambulisha.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako (Mb) na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) Kate Somvongsri wakiagana baada ya kufanya mazungumzo katika ofisi za Wizara Jijini Dodoma
……………………………………………….
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako leo Oktoba 28, 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkazi Mpya wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), Kate Somvongsri aliyefika ofisini kwake Jijini Dodoma kujitambulisha,
Katika mazungumzo hayo Waziri Ndalichako amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikishirikiana na Watu wa Marekani katika kuchochea maendeleo katika maeneo ya elimu, afya, haki za binadamu na utawala bora pamoja na masuala ya kiuchumi. Pia ameipongeza USAID kwa kuja na Programu ya Jifunze Uelewe inayolenga kuendeleza uboreshaji wa stadi za Kusoma, Kuandika na kuhesabu kwa wanafunzi wa elimu ya awali na msingi ambayo itatekelezwa katika mikoa ya Iringa, Mara, Mtwara, Ruvuma na Zanzibar.
Aidha, Waziri Ndalichako na Somvongsri wamekubaliana kushirikiana kwenye maeneo ya kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu ya msingi kwa kuongeza miundombinu, kushirikisha sekta binafsi katika kuboresha elimu, kuendeleza mafunzo ya walimu, kuboresha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika ufundishaji na ujifunzaji pamoja na kuhamasisha masuala ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu.
Mkurugenzi huyo pia ameahidi kusaidia kuiunganisha wizara na Mradi wa Global Book Alliance kwa ajili ya kuwezesha upatikanaji wa vitabu vya ziada katika shule za Msingi nchini.