Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi ambaye pia ni mhamasishaji wa kitaifa wa mpango wa jamii shirikishi na harakishi wa elimu na uhamasishaji wa chanjo dhidi ya UVIKO – 19 akitoa elimu ya chanjo hiyo kwa watumishi wa afya wa hospitali ya taifa ya magonjwa ya akili Mirembe na wanafunzi wa chuo cha uuguzi Dodoma kilichopo chini ya hospitali hiyo.
Watumishi wa afya wa hospitali ya taifa ya magonjwa ya akili Mirembe na wanafunzi wa chuo cha uuguzi Dodoma kilichopo chini ya hospitali hiyo wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi ambaye pia ni mhamasishaji wa kitaifa wa mpango wa jamii shirikishi na harakishi wa elimu na uhamasishaji wa chanjo dhidi ya UVIKO – 19 wakati akitoa elimu ya chajo hiyo.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali ya taifa ya magonjwa ya akili Mirembe Dkt. Japhet Swai akizugumza na wafanyakazi wa hospitali hiyo mara baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi ambaye pia ni mhamasishaji wa kitaifa wa mpango wa jamii shirikishi na harakishi wa elimu na uhamasishaji wa chanjo dhidi ya UVICO – 19 kumaliza kutoa elimu ya chanjo kwa watumishi wa hospitali hiyo na wanafunzi wa chuo cha uuguzi Dodoma kilichopo chini ya hospitali ya Mirembe.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi ambaye pia ni mhamasishaji wa kitaifa wa mpango wa jamii shirikishi na harakishi wa elimu na uhamasishaji wa chanjo dhidi ya UVIKO – 19 akizugumza na watoa chanjo hiyo kutoka ofisi ya jijini Dodoma mara baada ya kumaliza kutoa elimu ya chanjo dhidi ya UVICO – 19 kwa watumishi wa afya wa hospitali ya taifa ya magonjwa ya akili Mirembe na wanafunzi wa chuo cha uuguzi Dodoma.
Picha na JKCI
………………………………………………………..
Na Mwandishi Maalum – Dodoma
Watumishi wa afya nchini wametakiwa kujitokeza kwa wingi kuchanja chanjo dhidi ya UVIKO – 19 kwani wapo katika nafasi kubwa ya kupata maambukizi ya ugonjwa huo kupita wagonjwa wanaowahudumia ukilingaisha na watu wengine.
Rai hiyo imetolewa leo jijini Dodoma na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi wakati akitoa elimu ya chanjo kwa watumishi wa afya wa hospitali ya taifa ya magonjwa ya akili Mirembe na wanafunzi wa chuo cha uuguzi Dodoma kilichopo chini ya hospitali hiyo.
Prof. Janabi ambaye pia ni mhamasishaji wa kitaifa wa mpango wa jamii shirikishi na harakishi wa elimu na uhamasishaji wa chanjo dhidi ya UVIKO – 19 alisema mwitikio wa wataalam wa afya kutoka Hospitali ya Taifa ya Magonjwa ya akili Mirembe umekuwa mkubwa na elimu waliyoipata itawasaidia kuwa mabalozi wazuri katika jamii zinazowazunguka na kuwafanya wananchi kupata taarifa sahihi kuhusu chanjo ya UVIKO – 19 .
“Wataalam wa afya ukiacha kwamba tupo hospitali kwa muda mwingi pia tupo katika nafasi kubwa ya kupata ugonjwa wa UVIKO – 19 hii ni kutokana na mazingira tuliyonayo hivyo kuziweka familia zetu katika hatari ya kupata ugonjwa huu, ni vyema tukapata taarifa sahihi na kuwa mstari wa mbele kuchanja na kulinda afya zetu”, alisema Prof. Janabi
“Leo hii nimetoa elimu kwa wahudumu wa afya kwasababu tuna imani kubwa wafanyakazi wa afya wakiwa na uelewa wa kutosha na kujitokeza kuchanja itatoa motisha pia kwa jamii kujitokeza kwa wingi lakini pia watakuwa wahamasishaji wakubwa kutoa elimu hiyo ya kisayansi kwa wananchi wanaowazunguka”, alisema Prof. Janabi.
Kwa upande wake kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Magonjwa ya akili Mirembe Dkt. Japhet Swai alisema wafanyakazi wa Mirembe wamekuwa na shauku ya kupata elimu kama waliyoipata kupitia Prof. Janabi ambayo kwa hakika itafuta rekodi ya wataalam kutoka Hospitali ya Mirembe ya kuwa nyuma katika suala ya kuchanja chanjo ya UVIKO – 19.
“Kati ya watumishi 190 tulionao watumishi waliochanja hadi sasa ni 28 tu kutokana na maswali mengi ambayo yalikuwa hayajapatiwa ufumbuzi lakini sasa ujio wa Prof. Janabi umekuwa ni bahati kwa watumishi wa Mirembe kupatiwa ufumbuzi wa maswali waliyokuwa nayo, naamini sasa watajitokeza kuchanja na kuelimisha jamii inayowazunguka”, alisema Dkt. Swai
Naye daktari bingwa wa magonjwa ya akili kutoka Hospitali ya Taifa ya Magonjwa ya akili Mirembe na Mkuu wa Kitengo cha Mafunzo na Tafiti Innocent Mwombeki alisema amepata elimu mpya kuhusu chanjo ya UVIKO – 19 ambayo sasa anaweza kuitoa na kuipeleka kwa wafanyakazi wenzake ili kuhakikisha kuwa wafanyakazi wote wamejikinga na ugonjwa huo pamoja na kujitokeza kuchanja.
“Maswali mengi ambayo watu wamekuwa nayo katika jamii kuhusu chanjo ya UVIKO – 19 leo tumepata majibu yake kupitia elimu iliyotolewa na Prof. Janabi hivyo naamini elimu hii itasaidia sana kupunguza hofu waliyokuwa nayo wafanyakazi wa afya na kuwapa motisha ya kujitokeza kuchanja”, alisema Dkt. Mwombeki.
Naye mwanafunzi wa udaktari bingwa wa magojwa ya akili wa mwaka wa pili katika Hospitali ya Mirembe Suluma Aslan alisema chanjo ya UVIKO – 19 ilivyoingia nchini aliogopa kuchanja kutokana na hali yake ya ujauzito aliyokuwa nayo kwamba ungemletea shida yeye pamoja na mtoto wake lakini baada ya elimu sahihi ya chanjo amekuwa ni miongoni mwa watu waliochanja siku ya leo.
Takwimu zinaoesha kuwa hadi sasa chanjo karibu bilioni 6.9 zimeshatolewa na nusu ya dunia imeshachanja wakati Bara la Afrika asilimia 3 ya watu ndio waliopata chanjo.