Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Agnes Kijazi akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam kuelezea utabiri wa mvua za msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka. Kulia ni Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri Mamlaka ya Hali ya Hewa TMA, Dkt. Hamza.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Agnes Kijazi akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam kuelezea utabiri wa mvua za msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka. Kulia ni Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri Mamlaka ya Hali ya Hewa TMA, Dkt. Hamza.
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) leo imetoa utabiri wa mvua za msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka huku ikionesha mikoa mingi ya maeneo hayo yakitarajiwa kuwa na mvua za chini ya wastani hadi wastani.
Akizungumza na vyombo vya habari kutoa utabiri huo, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Agnes Kijazi ameitaja mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Singida, Dodoma, Rukwa, Songwe, Mbeya na Iringa kuwa inatarajia kuwa na mvua za chini ya wasta hadi wastani.
Dk. Kijazi amesema kwa mikoa ya Njombe, Ruvuma, Lindi, Mtwara na kusini mwa mkoa wa Morogoro inatarajiwa kuwa na mvua za wastani hadi chini ya wastani, huku akiitaja mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Singida, Dodoma, Rukwa, Songwe, Mbeya na Iringa ikitarajia kupata mvua za chini ya wastani hadi wastani.
“…Aidha, Vipindi virefu vya ukavu vinatarajiwa kati ya mwezi Novemba, 2021 na Januari, 2022. Ongezeko kidogo la mvua linatarajiwa mwezi Machi 2022, mvua zinatarajiwa kuanza katika wiki ya tatu ya mwezi Novemba, 2021 katika maeneo mengi na kuisha kati ya wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Aprili, 2022.” Alieleza Mkurugenzi, Dk. Kijazi.
Alibainisha kuwa mwelekeo wa msimu wa vuli kwa miezi ya Oktoba hadi Disemba 2021 kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua ikiwemo mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara, Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Dar es Salaam, kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, Pwani kijumuisha kisiwa cha Mafia mvua zinatarajiwa kuwa za chini ya wastani hadi wastani.
Tayari TMA imetoa ushauri na tahadhari kwa wadau wa sekta mbalimbali wanaotumia taarifa za hali ya hewa katika utekelezaji wa majukumu yao kama vile kilimo na usalama wa chakula, mifugo na uvuvi, maliasili, wanyamapori na utalii, pamoja na sekta ya afya ili kuchukua taadhari kuepusha athari zozote zitakazoweza kujitokeza.