*********************************
Na Mwandishi wetu,
Tanzania inatarajia kuwakilisha taarifa yake ya utekelezaji wa haki za binadamu na kufanyiwa tathimini chini ya mfumo wa Umoja wa Mataifa kwa kipindi maalum (Universal Periodic Review-UPR) huko Geneva kuanzia tarehe 1-12 Novemba 2021.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula(Mb) ameyasema hayo Mkoani Morogoro wakati akifungua mafunzo ya watendaji waandamizi wa Taasisi za Serikali zinazosimamia haki za binadamu kuhusu kuongeza utekelezaji wa tamko la Marrakesh.
Ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kutekeleza wajibu wake wa kikatiba na kutekeleza wajibu ilionao kupitia Mikataba ya Kimataifa na kikanda ambayo imeridhia na kwamba inatambua umuhimu wa watetezi wa haki za binadamu kama wadau wakubwa wa kulinda, kukuza na kudumisha haki za binadamu.
Balozi Mulamula amesema hatua ya Tume ya haki za binadamu na Utawala Bora ya Tanzania kutajwa kuwa miongoni mwa Tume bora 23 Barani Afrika kwa kusimamia na kuzingatia mikataba ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa nay a kujivunia na kwamba Serikali itaendelea kusimamia na kutekeleza mikataba hiyo hapa nchini.
Pia amesema Serikali inawategemea watetezi wa haki za binadamu kama “Whistleblowers” pale kunapotokea ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na Taasisi za Serikali au watu binafsi na pia katika kubaini matumizi mabaya ya madaraka kwa Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali.
Balozi Mulamula ameongeza kuwa Serikali ineheshimu tamko la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kijamii na kisiasa ambayo inatoa wajibu kwa Serikali kulinda na kudumisha haki za binadamu pamoja na kuwalinda watetezi wa haki za binadamu.
Ametoa kwa wadau kushirikiana ili kuondoa mtazamo hasi uliopo duniani kote ya watetezi wa haki za binadamu kuonekana kama adui wa Serikali na Sio walinzi wa watu kwamba Serikali inatambua wajibu wa kuweka mazingira wezeshi ya kisheria na kitaasisi ya kuhakikisha kuwa watetezi wa haki za binadamu wanaweza kufanya kazi zao kwa uhuru.
Ameishukuru Wizara ya Katiba na Sheria na wadau wote kwa kushiriki ipasavyo kwenye maandalizi ya Taarifa hiyo ambayo inaenda kukamilisha wajibu wa Tanzania kutoa taarifa kuhusu utekelezaji wa haki za binadamu nchini.
Awali akizungumza wakati akimkaribisha Balozi Mulamula Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Jaji Mstaafu Methew Mwaimu amesema tume anayoingoza itaendelea kusimamia na kutekeleza kikamilifu mikataba ya haki za binadamu na utawala bora ya Kitaifa,Kikanda na Kimataifa.
Ameishukuru Serikali kwa ushirikiano inayoitoa kwa tume hiyo jambo la linaloiwezesha kuendelea kutekeleza majukumu yake kikamilifu.