Mkurugenzi wa Ushirika wa Wanawake Wajasiriamali (GCI,) Fatma Kange, Mwanzilishi wa shirika la ‘Najim Foundation’ (NACHO,) Kibibi Bayaka na mwenyekiti wa shirika hilo Jane Wasira pamona na wanachama wengine wa shirika hilo wakimuangalia Asia Hamza dada wa Sumaia Hamza ambaye ni mlemavu mara baada ya kukabidhiwa baiskeli yake katika hafla iliyofanyika katika hoteli ya Lamada Ilala jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Ushirika wa Wanawake Wajasiriamali (GCI,) Fatma Kange, Mwanzilishi wa shirika la ‘Najim Foundation’ (NACHO,) Kibibi Bayaka wakimkabidhi baiskeli maalum Sumaia Hamza ambaye ni mlemavu katika hafla iliyofanyika katika hoteli ya Lamada Ilala jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Ushirika wa Wanawake Wajasiriamali (GCI,) Fatma Kange, Mwanzilishi wa shirika la ‘Najim Foundation’ (NACHO,) Kibibi Bayaka wakikata utepe kuzindua vifaa maalum kwa ajili ya watoto wenye ulemavu katika hafla ya kuwakabidhi iliyofanyika kwenye hoteli ya Lamada Ilala jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi wa Ushirika wa Wanawake Wajasiriamali (GCI,) Fatma Kangeakitoa hotuba yake katika hafla hiyo.
Baiskeli maalum zilizokabidhiwa kwa watoto wenye ulemavu na shirika la ‘Najim Foundation’ (NACHO,)
Mkurugenzi wa Ushirika wa Wanawake Wajasiriamali (GCI,) Fatma Kange akikata keki maalum iliyoandaliwa katika hafla hiyo.
……………………………………
SHIRIKA La ‘Najim Foundation’ (NACHO,) limepongezwa kwa jitihada za kuwasaidia watoto wenye ulemavu pamoja na walezi wao wa msingi jambo linalounga mkono juhudi na azma ya Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa akisisitiza jamii, mashirika yasiyo ya Serikali na kimataifa kushiriki katika kusaidia watu wenye ulemavu hasa katika mahitaji ya msingi ikiwemo vifaa mwendo na elimu.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi rasmi wa shirika hilo hafla iliyoenda sambamba na ugawaji wa vifaa mwendo wa watoto 40 wenye ulemavu, Mkurugenzi wa Ushirika wa Wanawake Wajasiriamali (GCI,) Fatma Kange amesema shirika hilo limekuwa ya mfano na mwavuli utakaowasaidia wanawake wanaotunza watoto wenye ulemavu kusema changamoto na uhitaji wao ambapo kila mmoja katika jamii, Serikali, Asasi za kiraia na mashirika ya Kimataifa ana wajibu wa kuonesha ushiriki kwa kuhakikisha watoto hao wanapata mahitaji ya kimsingi.
”Safari ya wanawake huwezi kuitafuta, kuna mapito mengi na changamoto nyingi zilizojificha, NACHO imeanzisha mwavuli imara na salama kwa kusema changamoto zetu kama walezi wa watoto wetu wenye mahitaji mengi…. tuwatumie NACHO kueleza changamoto zetu na kuangalia namna ya kuzitatua pamoja kwa kushirikiana na Serikali na asasi za kiraia na kimataifa na kuwawezesha walezi wao wa karibu juu ya namna ya kujikwamua kiuchumi na sio kuwatumia watoto kama nyenzo ya kupata kipato.” Amesema.
Amesema Serikali ya awamu tano imejibainisha wazi juu ya azma ya kutetea watu wenye ulemavu na wanawake kwa ujumla na kuitaka jamii kwa ujumla kutowaficha watoto hao hasa katika kipindi hiki ambapo Taifa linaelekea katika sensa ya watu na makazi.
”Mwaka ujao kutakuwa na zoezi la sensa ya watu na makazi, wazazi, walezi na jamii kwa ujumla tutumie fursa hii kutoa takwimu sahihi tuwatoe watu wenye mahitaji muhimu ili Serikali iweze kuwasaidia mahitaji ya msingi.” Ameeleza.
Kwa upande wake mwenyekiti wa shirika hilo Jane Wasira amesema, mwanzilishi wa shirika hilo Kibibi Bayaka aliona changamoto wanazopitia wanawake wanaolea watoto wenye ulemavu kupitia kijana wake mwenye ulemavu Najim (26,) na kuanzisha shirika hilo ili kuweza kuwakutanisha wanawake hao, kujadili changamoto zinazowakabili na kutafuta namna ya kuzitatua.
” Shirika la Najim itatoa huduma za day care kwa watoto wenye ulemavu kuanzia wachanga hadi miaka 16 ambapo watakutana na kutojihisi wapo peke yao na wakiwa hapo kutakuwa na walimu watakaowafundisha masuala mbalimbali na madaktari wa mazoezi licha ya hayo vifaa mwendo, vifaa vya choo, vifaa vya kusimamia na vifaa vyaa mazoezi vitatolewa kwa watoto wanaotoka katika hali duni.” Amesema.
Vilevile amesema pia kwa wanawake waliotelekezwa na watoto hao kuna mpango wa kutoa ruzuku na mafunzo ya ujasiriamali ili waweze kushiriki shughuli za kijamii na kiuchumi ili kukomesha shughuli za kuomba barabarani jambo ambalo huwaathiri watoto hao kisaikolojia.” Amesema.
Awali Mwanzilishi wa shirika hilo Kibibi Bayaka aliwataka wanawake na walezi wa watoto hao kutokata tamaa na kutowatumia watoto hao katika shughuli za kuomba barabarani na kuahidi ushirikiano katika kutatua changamoto zinazowakabili na kuwashauri kuutumia vyema mwaka ujao katika sensa ya watu na makazi kwa kutoa takwimu sahihi ili waweze kupata mahitaji muhimu kutoka kwa Serikali inayoongozwa na Rais mwanamke na mpigania haki za wanawake na walemavu Samia Suluhu Hassani.