Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza wakati wa tukio la uzinduzi wa mradi wa Kanisa Katoliki wa mapambano dhidi ya UVIKO 19, unaofadhiliwa na Serikali ya Marekani, katika hospitali ya Cardinal Rugambwa iliyopo Ukonga, Dar es Salaam, Oktoba 27, 2021. Kulia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga na katikati ni Balozi wa Marekani nchini Donald Wright. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikata utepe kuzindua mradi wa Kanisa Katoliki wa mapambano dhidi ya UVIKO 19, unaofadhiliwa na Serikali ya Marekani, katika hospitali ya Cardinal Rugambwa iliyopo Ukonga, Dar es Salaam, Oktoba 27, 2021. Wengine kutoka kushoto ni Jane Manyahi Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Cardinal Rugambwa na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na uzazi, Balozi wa Marekani nchini Donald Wright, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Dkt. Godwin Mollel na kulia ni Mbunge wa Ukonga Jerry Slaa. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiagana na Balozi wa Marekani nchini Donald Wright wakati wa tukio la uzinduzi wa mradi wa Kanisa Katoliki wa mapambano dhidi ya UVIKO 19, unaofadhiliwa na Serikali ya Marekani, katika hospitali ya Cardinal Rugambwa iliyopo Ukonga, Dar es Salaam, Oktoba 27, 2021. kushoto ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga na watatu kushoto ni Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam Stephano Msomba. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa wito kwa viongozi wa dini nchini waendelee kuiunga mkono Serikali katika mapambano ya UVIKO 19 sambamba na kuelimisha umma umuhimu wa kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo.
Amesema hadi kufikia tarehe 22 Oktoba 2021, jumla ya wananchi 981,297 walikuwa wamechanjwa na jumla ya wagonjwa 26,154 na vifo 725 vilitolewa taarifa tangu ugonjwa huo uliporipotiwa kuingia nchini kwa mara ya kwanza tarehe 19 Machi 2020.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatano, Oktoba 27, 2021) wakati akizindua Mradi wa Mpango wa Kanisa Katoliki wa Mapambano dhidi ya UVIKO-19 katika Hospitali ya Cardinal Rugambwa iliyopo Ukonga, Dar es Salaam.
Mradi huo unatekelezwa kupitia vituo 12 vya kutolea huduma za afya vya Kanisa Katoliki vilivyopo kwenye maeneo mbalimbali nchini ili kusaidia kujaziliza kazi kubwa inayofanywa na Serikali katika kudhibiti maambukizi ya UVIKO 19.
Amesema licha ya Tanzania kuudhibiti mlipuko huo, bado ugonjwa upo na wagonjwa pamoja na vifo vinavyotokana na ugonjwa huo vinaendelea kufuatiliwa na kutolewa taarifa huku Serikali ikitekeleza afua mbalimbali za kupambana na janga hilo pamoja na kuimarisha uchumi na huduma za jamii.
“Hivyo basi, tuendelee kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa huu kwa kujijengea utamaduni wa kuvaa barakoa safi na salama, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono pamoja na kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima.”