Mwenyekiti wa Umoja wa wadau wa maendeleo Kiserian ,Lonyamali Morwo akimkabithi vitabu hivyo Mkuu wa shule ya Sekondari Kiserian ,Mary Malesa shuleni hapo (Happy Lazaro)
Diwani wa kata ya Mlangarini mkoani hapa, Zebedayo Laizer akizungumza katika hafla hiyo ya kupokea msaada wa vitabu katika shule ya Sekondari Kiserian iliyopo kata ya Mlangarini kutoka kwa umoja huo .(Happy Lazaro)
***************************
Happy Lazaro,Arusha
Arusha.Umoja wa wadau wa maendeleo Kiserian kata ya Mlangarini wilayani Arumeru wamechangia vitabu 45 vya kujisomea kwa ajili ya kuinua kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Kiserian .
Aidha kupatikana kwa vitabu hivyo vya masomo yote ni juhudi zilizofanywa na Diwani wa kata hiyo, Zebedayo Laizer aliyewaomba wadau hao kuchangia shule hiyo ambayo bado ni mpya na inakabiliana na changamoto mbalimbali .
Akizungumza wakati wa kukabithi vitabu hivyo shuleni hapo,Diwani wa kata hiyo amesema kuwa, shule hiyo ambayo ina hadi kidato cha pili imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali kutokana na kuwa ni mpya na idadi ya wanafunzi wanaohitaji huduma ni wengi shuleni hapo.
Amesema kuwa, alitembelea shule hiyo na kuweza kubaini inakabiliwa na changamoto ya vitabu kwa ajili ya wanafunzi kusomea ,ndipo alipotafuta wadau kwa ajili ya kusaidia shuleni hiyo na kuweza kufanikisha changamoto hiyo.
“Kwa kweli nawashukuru Sana wadau hawa ambao ni umoja wa wanafunzi waliosoma hapa Kiserian kwa namna ambavyo wameweza kusikia wito wangu na kuja kuisaidia hii shule na hii itasaidia Sana kiwango cha ufaulu kuongezeka shuleni hapa na bado naendelea kutafuta wadau wengine kwa ajili ya kuendelea kusaidia shule hii na shule nyingine za kata hii”amesema Diwani.
Naye Mwenyekiti wa Umoja huo,Lonyamali Morwo amesema kuwa,wamefikia hatua ya kujichanga baadhi ya wanafunzi waliosoma shule ya msingi Kiserian miaka mingi kutokana na changamoto walizokuwa wakikabiliana nazo wakiwa shuleni ndipo walipoona umuhimu wa kurudisha fadhila kwa kile kidogo walichokipata kwa ajili ya kusaidia wanafunzi shuleni hapo kuongeza kiwango Cha ufaulu.
Morwo amesema kuwa,lengo la kutoa vitabu hivyo ni ili kuwasaidia waalimu waweze kuandaa masomo wakiwa na vitabu sahihi huku wakiwezesha pia wanafunzi hao kuweza kuwa na vitabu vya ziada kwa ajili ya kujisomea na hatimaye kuondokana na changamoto hiyo ya upungufu wa vitabu.
“Umoja huu tumeamua kuungana na kuwa kitu kimoja kwani wengine wapo mikoa mbalimbali na tunawasiliana kwa njia ya mtandao tu, na tumedhamiria kuhakikisha tunaleta maendeleo katika kata hii ambapo tumejipanga kusaidia maswala ya afya,maji na hata elimu na hii ni ili kuisaidia Serikali kwani ina shughuli nyingi za kufanya .”amesema Morwo.
Naye Mkuu wa shule hiyo,Mary Malesa amesema kuwa, anamshukuru sana Diwani wa kata hiyo kwa kushirikiana na Umoja huo kwa kuwatatulia changamoto ya vitabu shuleni hapo kwani ilikuwa mojawapo ya changamoto iliyokuwa ikiwakabili kwa muda mrefu shuleni hapo.
Amesema kuwa, hapo awali kitabu kimoja kilikuwa kikitumiwa na wanafunzi watano ambapo kupitia msaada huo wa vitabu imesaidia Sana kwani kwa Sasa hivi wanafunzi watatu watasoma kitabu kimoja ,hivyo aliwataka wadau wengine kuendelea kujitokeza kwa wingi katika kuisaidia shule hiyo ambayo ina hadi kidato cha pili.